Share this:

Maswali ya UFAHAMU

1.  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

Panografia ni tendo, maandishi, picha au michoro inaoonyesha au kueleza uchi wa mtu au vitendo vya ngono kwa ajili ya kuchochea ashiki ya kuifanya. Mambo haya machafu huwasilishwa ana kwa ana kupitia sinema, magazeti, vitabu, muziki, televisheni, tovuti na kanda za kunasia picha na sauti.

Ponografia imekuwepo tangu jadi, hasa katika nchi za magharibi. Lakini sasa limekuwa tatizo sugu. Hii ni kwa sababu imeenea kote ulimwenguni mithili ya moto mbugani wakati wa kiangazi. Kuenea kwake kumechangiwa na mambo kadha wa kadha. Mchango mkubwa zaidi ukiwa umetokana na kuimarika kwa vyombo vya teknolojia ya habari na mawasiliano. Hata hivyo, kazi hii hubuniwa au kutengenezwa na makundi mbalimbali ya watu. Miongoni mwa hawa ni watu wasiojali maadili. Pili, kuna wale wenye matatizo ya kisaikolojia na kijamii. Wao hutengeneza na kueneza uchafu huu kwa lengo la kuvuruga madili katika jamii au kuchukiza wanajamii waadilifu.Kundi lingine ni lile la wanaoichukulia ponografia kama nyenzo ya kutosheleza ashiki zao. Kwa mfano, baadhi ya wanamuziki hutumia ponografia kuvutia wateja na hivyo kuzidisha mauzo yao.

Kushamiri kwa wimbi na uonyeshaji wa ponografia kuna athari kubwa kwa jamii hasa watoto. Ingawa watu wengine hudai picha hizi haziwaathiri, upo ushaihidi kuonyesha kuwa wale wanaotazama picha za ngono hupata matatizo. Lazima ieleweke kwamba kinachoonekana kwa jicho au kusikika kwa sikio huathiri fikira au hisia. Picha za matusi zinachangia kwa kisasi ikubwa kuharibu akili. Badala ya kuzingatia mambo muhimu kama vile masomo, watu huanza kutafakari mambo machafu.

Vijana wengi ni kama bendera, huyaiga wanayoyaona na kuyasikia. Hii ni tatizo linalowafanya kuacha mkondo wa maadili. Hivyo basi wengi hushawishiwa kuingilia shughuli za ngono mapema kabla hawajakomaa kimwili, kiakili na kihisia. Matokeo yake ni ukahaba, utendaji mbaya shuleni, mahudhurio mabaya darasani na mimba zisizotarajiwa. Vijana wengi huacha shule kabisa huku wengine wakiambukizwa magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kuwaletea mauti.

Yasemekana kuwa akili za binadamu hunasa zaidi mambo yanayowalishwa kwa picha na hivyo basi matusi haya yaweza kudumishwa katika kumbukumbu zao. Tabia mbaya kama vie ushoga, ubasha na usagaji huwa matokeo yake na hata matokeo ya vijana hugeuka wanapoanza kuiga mitindo mibaya ya mavazi yanayoanika uchi wao. Hali kadhalika, lugha, ishara na miondoko inayohusiana nanmgono huibuka. Yote haya yanakinzana na desturi za mwafrika. Si ajabu visa vya ubakaji vinaongezeka kuchapo. Utazamaji wa picha chafu aghalabu huandamana na maovu mengine kama vile unywaji pombe na matumizi ya vileo ambavyo huchochea uchu wa ngono na kuibua tabia za kinyama.

Kuendelea kuzitazama picha hizi huzifanya nishai na hisia za watu kuwa butu, huondoa makali kiasi kwamba hata katika uzima mtu hupoteza mhemko na kugeuswa kuwa mtegemezi wa ponografia. Tatizo hili linaenea kwa vishindo mjini na vijijini. Ipo haja ya dharura kuikinga jamii kutokana na malezi haya yasiyo na kizuizi.

Kuuongeza ufahamu wa umma wote kuhusu uovu wa picha hizi, watu wazima kuwajibika kwa kuwalinda na kuwahimiza vijana kuhusu maovu haya na wale wenye midahilishi, video na sinema kutowaruhusu vijana kutazama uchafu huu kunaweza kuwa maana ya kuyakinga au hata kuyaepuka madhara ya ponografia. Ni sharti pia sheria izuie na kupiga marufuku utengenezaji na uenezaji wa upungufu huu. Bila shaka, sheria na hatua kali za ziweze kuchukulia dhidi ya waivunjao. Hali kadhalika, wazazi wasijipweteke tu bali wawaelekeze watoto wao ipasavyo na ila mtu alitekeleze jukumu lake.

 

Maswali

(a) Yape makala uliyosoma anwani mwafaka  

 (b) Toa sababu za kusambaa kwa uchafu unazozungumziwa katika taarifa

(c) ‘Bendera hufuata upepo’. Thibitisha ukweli wa usemi huu kulingana na makala

(d) Ni kwa nini ni muhimu kuwakanya vijana dhidi ya uchafu huu?

 (e) Ni hatua zipi zinazofaa kuchukuliwa dhidi ya aina ya uozo unaozungumziwa na mwandishi?  

ecolebooks.com

(f) Fafanua msamiati huu kimuktadha

(i) uchu …………………………………………………………………

   (ii) wasijipweteke …………………………………………………………….

(iii) nishai …………………………………………………………………

 

2.  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.
Ilikuwa Jumamosi. Nilifika nyumbani kwangu saa moja jioni. Tangu nistaafu miaka

miwili awali sikupenda kuchelewa Taarifa ya Habari.
Mwezi mmoja ukawa umepita tangu nipewe pesa za kiinua mgongo. Mwezi mmoja mzima nilikuwa katika shughuli za kulipa deni hapa na kulipa karo huku. Kuwekeza kwenye mradi ule na kununua hili. Sasa shilingi laki mbili tu zilikuwa zimesalia katika benki.
 Watu wengi walinishawishi nijaribu kilimo cha mahindi. Bei ilikuwa imeanza kuimarika. Katika taarifa ya habari jioni hiyo, Waziri wa Kilimo alitangaza bei mpya. Shilingi 1,500 kwa kila gunia. Nami nilikuwa naanza kuumakinikia mradi huu.
 Baaada ya taarifa, nilikoga, nikala na nikaenda kulala. Kwa sababu ya uchovu, usingizi ulinichukua mara moja.. Usingizini niliota. Katika ndoto niliutekeleza mradi wangu. Msimu huo wa kilimo nilitenga ekari kumu za shamba langu. Wataalamu walinishauri kuwa wakati mzuri wa kulima ni wa kiangazi. Mwezi wa Januari ulipoanza tu nilitafuta trekta na kulima. Malipo yalikuwa shilingi 1,200 kila ekari. Katikakati ya mwezi wa Machi, nilitafuta trekta la kutifua shamba tena kwa gharama ya shilingi 15,000 ekari zote kumi. Kufuatia ushauri wa manyakanga wa kilimo, nilipa shilingi elfu kumi na tatu kupiga shamba lote haro.
 Mwishoni mwa mwezi huo, nilienda mjini kutafuta pembejeo. Kwanza, nililipa shilingi 20,500 kwa magunia 15 ya mbolea. Kisha nilinunua magunia manne ya mbegu ya mahindi yenye uzani wa kilo 25 kwa shilingi 3,300 kila gunia. Mwezi wa Aprili ulipotimia tu, niliamua kupanda. Ili nipate mazao bora, nilipanda kwa tandazi. Gharama ilikuwa shilingi 1,000 kila ekari. Mvua ilinyesha vizuri na baada ya siku saba mahindi yalianza kuota. Ilifurahisha kuhesabu mistari ya kijani iliyonyooka. Hali hii iliwezekana tu baada ya kuajiri vijana wa kuwafukuza korongo na vidiri ili wasifukue mbegu mchangani.
 Baada ya mwezi mmoja, hatua ya kupalilia ilifika. Nilitafuta vibarua wa kupalilia. Malipo yalikuwa shilingi 700 kila ekari. Kumbe kupalilia kulichochea mtifuko wa mahindi. Punde yakawa yananifikia magotini. Hii ikawa ishara kuwa yanahitaji kumwagiwa mbolea ya kunawirisha iitwayo ‘amonia.’ Gharama yake ikawa shilingi1,300 kila gunia. Hivyo, nikalipa shilingi 19,500 kwa magunia kumi na matano..
 Mahindi yalibadilika kimiujiza. Ghafla tu yalirefuka na kunenepa mashina. Yalibadilika rangi yakapiga weusi. Shamba liligeuka likawa kama msitu wa rangi ya kijani iliyokolea. Wapita njia waliajabia mimea na juhudi zangu. Shamba langu sasa likawa kielelezo. Maafisa wa kilimo wakawa kila siwanawaleta wakulima wengine kujifunza siri ya ufanis wangu. Hapo nikaanza kuhesabu mavuno nitakayopata kukadiria faida. Nilipuuza kabisa ushauri wa wahenga kuwa ‘Usikate majani, mnyama hajauawa.’

Bila taarifa wala tahadhari mvua ikatoweka. Hayakupita majuma mawili mahindi yakaanza kubadilika. Juma moja baadaye mahindi yalinyauka. Badala ya mahindi, shamba likageuka la vitunguu vilivyochomwa na jua. Makasio yangu ya faida yaliyeyuka jinsi ufanyavyo moshi.
 Lakini ‘Muumba ndiye Muumbua.’ Siku moja mawingu yalitanda na mvua ikanyesha. Muda is muda mahindi yalianza kunawiri. Kumbe tukio lililonivunja moyo lilikuwa laja. Siku moja mvua kubwa ilinyesha. Asubuhi nilipotoka nje nilipigwa na butwaa. Barafu ilitapakaa pote. Shamba lilikuwa limetapakaa barafhuku majani ya mahindi yamechanika kama nyuzi. Niliugua. Baada ya wiki moja, nilipata nafuu. Nilipotazama upande wa shamba nikaona dalili za majani mapya ya mahindi yakianza kuchomoza. Maumbile ni kitu cha ajabu kweli.
 Muda si mrefu mahindi yalirudi hali yake tena, kisha yakakomaa. Harakati za kutafuta watu wa kuyakata na kuyakusanya zilianza. Gharama ya shughuli hii ikawa shilingi 5,000. Kuvuna, kusafirisha kutoka shamba na kukoboa kwa mashine magunia 200 yakachukua shilingi 20,500. Kufikia hapo nilikuwa nimetumia takribani shilingi 192,700. Gharama nyingine zilikuwa za usafiri, gharama ya dharura na usimamizi, usumbufu wangu binafsi, gharama ya magunia na kadhalika. Mahindi yalipokuwa tayari kwenye magunia nilifunga safari kwenda mjini kutafuta soko. Niliposhuka tu niliona gazeti. Habari motomoto siku hiyo ilikuwa: ‘MAHINDI GUNIA 900/=.’ Niligutuka usingizini.

 

 Maswali:

 a)  Andika kichwa mwafaka kwa kifungu hiki cha habari.  

 b)  Msimulizi alikuwa na kiasi gani cha pesa katika benki baada ya mradi kukamilika?

 1. Taja matatizo matatu yaliyotisha mradi wa msimulizi wa kukuza mahindi.
 2. Eleza maana ya methali zifuatazo:

(i) Usikate majani, mnyama hajauawa.

 1. Eleza mambo mawili yaliyosababisha msimulizi asipate faida alivyotarajia.  

 f)  Kwa nini msimulizi alisema maumbile ni kitu cha ajabu?  

 g)  Eleza maana ya:

(i) kiinua mgongo.

(ii) manyakanga wa kilimo.

 

3.  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.
Mtoto anapozaliwa huwa ni malaika wa Mungu. Hutaraji kuongozwa kwa kila njia ili awe mwana mwelekea. Jukumu la kulea mtoto huanzia nyumbani. Wako baadhi ya watu ambao wanaamini kuwa jukumu hili muhimu hutekeleezwa bora na mama; wengine husema kuwa ni jukumu la baba. Ni kweli kwamba mtoto huwa na mama yake kwa muda mrefu zaidi ya baba lakini kivuli cha baba hakikosi kumwandama na kumwathiri maisha yake.

Uongozi wa mama huanzia siku ya mwanawe kuingia ulimwenguni. Kwa hivyo, mama zaidi ya baba huwa ndiye chanzo cha
chemichemi ya maisha ya mwanawe. Mtoto kwa kawaida ana tabia ya kuiga kila jambo analoliona na kusikia na mambo ya awali ajifunzayo hutokana na mamaye.

Je; mtoto huiga kutokana na mama pekee? Kila utamaduni hasa huku kwetu Afrika, una taratibu zake zilizopangwa kuhusu malezi ya watoto. Kwa mfano; akina baba wengine wanaoishi maisha ya kijadi huonelea kwamba ni jukumu lao kuwalea watoto wa kiume. Kwa hivyo mvulana anayekulia katika mazingira haya akishachuchuka kiasi cha kujua lipi zuri lipi baya huanzia kuwa mtoto wa baba zaidi ya kuwa wa mama. Baba humuathiri mtoto wake kwa kumshauri kuhusu maneno ya kiada ya wanaume. Hupenda kukaa naye katika uga wake kwa kumshauri kuhusu maneno ya kiada ya wanaume huku akimkataza kukaa jikoni na kumsisitizia kuwa wanawake ni tofauti naye. Aidha, humfunza sifa kama vile ushujaa na uvumilivu kwa namna ambayo huona kuwa ni ya kiume. Pindi mtoto anapoonyesha tabia za kikekike, baba hujiandaa kuzitadaruki kwa kumkaripia. Baba hutaka kujiona mwenyewe katika hulka ya mwanawe.

Baba kama huyu humpa nafasi ndogo sana mkewe ya kumwongoza mtoto wake wa kiume kwa jambo lolote hata kama wakati mwingine ni la heri. Kwa upande mwngine baba huyu huwa na machache ya kuzungumza na bintiye kwa kuwa huona kuwa si stahili yake kufanya hivyo. Mtoto wa kike huachiwa mamake. Lakini kutokeapo jambo la kulipima mama huona linampita kimo, humwita baba kuingilia kati na aghalabu baba naye humwagiza dadake aje atoe suluhisho mwafaka.

Ulezi kama huu una nafasi yake katika jamii, lakini ni lazima tukiri kuwa pia unaendeleza maisha ya fawaishi na kuanzisha taasubi ambayo hatima yake ni mwanamke kukandamizwa na mwanaume. Wazazi walio na mwelekeo huu katika malezi yao hufikiri kuwa wataishi na watoto wao katika mazingira finyu na kwa hivyo waendelee kuwapulizia pumzi za kuhilikisha. Lakini ni sharti wakumbuke kuwa wao sio walezi peke yao na wala mtoto hawezi kuishi peke yake na kuwa na tabia ya kipekee. Leo ataishi kwao lakini kesho itambidi atoke aone ulimwengu. Kila atakapotia mguu ataona mambo mapya yatakayompa tajriba mpya na mawazo mapya ambayo aghalabu yataendelea kuiathiri hulka yake. Iwapo tabia alizozipata kwa wazazi wake hapo awali zilikuwa na misingi isiyokuwa madhubuti na mielekeo finyu, zinaweza kuwa pingamizi katika maingiliano yake na watu wengine. Mambo haya yanatuelekeza katika kufikiri kwamba maisha ya siku hizi hayaruhusu ugawaji wa kazi ya malezi ya namna ya baba na mama wa kijadi. Baba na mama ni walezi wa kwanza ambao kwa pamoja wanapaswa kuwaelekeza watoto wao katika maisha ya ulimwengu uliojaa bughudha na ghururi. Ni lazima wazazi watambue tangu awali kuwa katika malezi hakuna cha ubaguzi. Hakuna, mambo ajifunzayo mtoto wa kiume ambayo hayamhusu mtoto wa kike. Uvumilivu, bidii, utiifu na kadhalika ni sifa zinazomwajibikia kila mtoto kama vile upishi, ukulima na usafi. Mwanamke tangu azali ameumbwa kuwa mama na haipasi kulazimishwa kuchagua baina ya mtoto wa kike na kiume. Mapenzi na wajibu wa wazazi yapaswa yasiwe na mipaka bali yawe maridhawa kwa watoto wote.

 

Maswali

 (a) Toa kichwa mwafaka cha makala haya

(b) Kulingana na kifungu hiki, taja mambo mawili ambayo yanaweza kuwa hatari kwa

malezi ya watoto

(c) Kwa nini baba humpa nafasi ndogo sana mkewe ya kumwongoza mtoto wa kiume katika

jambo lolote hata kama wakati mwingine ni la heri

(d) Eleza mambo mawili ambayo ni ya manufaa katika ulezi jadi

 (e) Kulingana na makala haya, ushahidi gani unaonyesha kwamba kuna kutegemeana

katika ulezi jadi?  

(f) Taja sifa mbili ambazo baba humfundisha mwana wa kiume

 (g) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika kaktika kifungu hiki:

  (i) Chanzo cha chemichemi

  (ii) Akishachuchuka  

  (iii) Hulka.

 

4.  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

Habari kuwa watoto chini ya miaka mitatu ‘huwindwa’ kitandani na kuraushwa na wazazi wao waende shuleni mwendo wa saa kumi na moja asubuhi ni za kusikitisha.

Kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa elimu ya watoto wachanga (ECD), watoto hao hutakikana kuwa darasani kabla ya saa kumi na mbili asubuhi.

Wanapowasili wao huanza kufukuza ratiba ya masomo ambayo huwapatia muda mfupi mno wa kula, kucheza, kupumzika na hata kuchunguza afya na usalama wao.

Badala ya kuondoka mapema kuelekea nyumbani, wengi wao hufika saa za usiku pamoja na wazazi wao wakitoka kazini. Wanapowasili nyumbani wanapaswa kuoga na kupata chakula cha jioni kwa pupa ili wafanye mazoezi waliyopewa na walimu wao.

Mazoezi hayo huwa ya masomo yote matano huku kila somo likiwa na zaidi ya maswali thelathini. Badala ya kupumzika mwishoni mwa juma, watoto hao huhitjika kuhudhuria shule siku nzima ya Jumamosi. Jumapili wanatakiwa Kanisani na hali hii hujirudia mpaka muhula umalizike. Ikiwa ulidhani watapewa nafasi ya kupumzika wakati wa likizo , umekosea kwa sababu watoto hao huhitajika kuhudhuria shule. Hili limekuwa likiendelea hata baada ya Wizara ya Elimu kupiga marufuku kusomesha wakati wa likizo.

Wazazi-hasa wale wanaofanya kazi mijini- wamekuwa wakiunga mkono mtindo huu kwa sababu unawaondolea mzigo wa malezi na gharama ya kuwaajiri walezi.

Wataalamu wanasema matokeo ya hali hii ni watoto wakembe wenye afya na maadili
mabaya kutokana na kuchanganyishwa akili na walimu wanaowataka wajue kila kitu wakiwa na umri mdogo.

Kuwashinikiza
watoto wakembe wahudhurie shule na zaidi ya hayo wajue kila kitu kuna madhara mengi. Kwanza kabisa, kuraushwa kwa watoto macheo waende shule kunawanyima fursa ya kulala na kupumzika. Utafiti unaonyesha kuwa watoto wanahitaji kulala na kupumzika kwa zaidi ya saa 12 kwa siku. Hii ina maana kuwa mbali na muda mfupi wanaolala na kupumzika mchana kutwa, watoto wanapaswa kutumia usiku mzima kwa usingizi.

Hii huwasaidia kukua wakiwa na afya nzuri hasa kiakili. Matokeo ya kuwarausha watoto hao waende shule saa hizo huwafanya wakose furaha mbali na kuwafanya wachanganyikiwe kiakili.

Pili, kuwalazimisha watoto wakae darasani kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni huwa kunawanyima fursa ya kucheza na kutangamana. Wataalamu wa afya ya watoto wanapendekeza kuwa watoto wachanga wanapaswa kucheza ili viungo vya miili yao kama moyo, akili, mapafu na kadhalika vifanye kazi vizuri.

Kinyume na watu wazima ambao hufanya kazi nzito nzito na kuwawezesha kufanya mazoezi, watoto huwa hawafanyi kazi hizo. Wazazi na walimu wanapaswa kufahamu kuwa kazi ya watoto ni mchezo na wana kila haki ya kupewa furaha ya kucheza wakiwa shuleni na hata nyumbani.

Tatu, wazazi wengi ambao hufurahia kuwaachia walimu jukumu la kuwalea watoto wao huku wao wakiwa kazini huwa wanasahau kuwa sio kila mwalimu ana maadili yanayopaswa kuigwa na mwanawe. Ingawa tunawatarajia walimu wawe mifano bora ambayo inaweza kuigwa na kila mtu, ukweli ni kwamba baadhi ya walimu hawajui maana wala hawana maadili. Hatari ni kwamba watoto wakembe
husoma kwa kuiga wakubwa wao na ikiwa walimu wanaoshinda nao shule wamepotoka kimaadili, kuna uwezekano mkubwa wa watoto hao kupotoka pia. Hii ndiyo sababu wazazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa wanawao tabia mbaya ambazo hawaelewi zilipotoka.

Kila mzazi anayejali maisha ya mwanawe anapaswa kutekeleza jukumu lake la kumlea na kumwelekeza jinsi anavyotaka akue. Ni kinaya kuwa wanawatarajia wanawao wawe na tabia na maadili kama yao ilhali hawachukui muda wa kukaa nao na kuwaelekeza.

Nne, kuwawinda, kuwaamsha, kuwaosha na kuwalazimisha watoto waende shule kila siku hata ingawa hawataki huwa kunawafanya wawe wategemezi wasioweza kujipangia na kutekeleza mambo kivyao.


(TAIFA LEO, IJUMAA, FEBRUARI 5, 2010)

  MASWALI.

(a) Ipe taarifa anwani mwafaka

 (b) Mwandishi anatoa maoni gani kuhusu ratiba ya masomo?

(c) Eleza athari za mfumo wa elimu unaoangaziwa hapa

(d) Ni ushauri upi unaotolewa kwa wazazi ?

(e)Taja mbinu zozote mbili za lugha alizotumia mwandishi

 (f) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika taarifa.

   (i) ‘huwindwa’ kitandani

(ii) Maadili

(iii) Kuwashinikiza

 (iv) Wakembe…  

 

 

5. Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali. Ufisadi ni uhalifu unaohusu kuzitumia njia za ulaghai kujipatia pesa, mali au vitu hasa vya umma.

Nchini Kenya ufisadi hujitokeza kwa njia mbalimbali na kila mojawapo ina athari zake. Kwa mfano kuna maafisa wa serikali wajipatiao pesa kwa kuuza stakabadhi za serikali kama vile pasi, vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya kumiliki mashamba, vitambulisho n.k. kwa raia, kuna hatari kubwa kwa sababu watu wasio raia wa Kenya wameweza kusajiliwa kama wakenya na kuendeleza uhalifu kama ugaidi, wizi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Wengine hujipatia vibali vya kufanya kazi na kuajiriwa kazi ambazo zingefanywa na wakenya. Hii imechangia ongezeko la uhaba wa kazi nchini.

Watumizi wengine wa umma huuza mali ya serikali kama vile magari nyumba na ardhi na kufutika pesa za mauzo mifukoni mwao. Wengine wao hujinyakulia na kufanya vitu hivyo kuwa mali yao. Ufisadi wa aina hii umegharibu serikali kiasi kikubwa cha fedha. Serikali imelazimika kununulia maafisa wake magari baada ya muda mfupi, kulipia wafanyi kazi wake kodi za nyumba na kukosa viwanja vya upanuzi na ujenzi wa shule hospitali, vituo vya polisi na taasisi zingine maalumu.

Baadhi ya wataalamu kama madaktari huiba dawa kutoka hospitali za umma kupeleka vituo vyao vyaafya. Pia hutumia wakati wao mwingi katika kazi zao za kibinafsi na kuwaacha wagonjwa katika hospitali za umaa wakihangaika. Sio madaktari tu, kuna masoroveya, whandisi, mawakili, walimu na mahesibu ambao hukwepa majukumu yao serikalini na kufanya kazi za kibinafsi.. Wengine wasio wataalam huendesha biashara za aina tofauti, na huku wanaendelea kupokea mishahara.

Wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo na shule bora za umma na hawakuhitimu wakati mwinginehulazimika kusalimu amri na kutoa hongo hili wapate nafasi za kusoma. Kiasi cha pesa kinachohitajika huwa kikubwa hivi kwamba ni wachache humudu hizo rushwa. Wale wasiojimudu kifedha hubaki wakilia ngoa. Kuna wazazi ambao hutumia vyeo vyao na ‘undugu’ kupata nafasi zilizotajwa, jambo ambalo huwanyima wanafunzi werevu kutoka jamii maskini nafasi ya kupata elimu. Matokeo huwa ni kuelimisha watu wasiostahili na ambao mwishowe hawaziwezi kazi wanazosomea wakihitimu na kuanza hudumia jamii.

Ufisadi umekita mizizi na kushamiri katika sekta za umma za kibinafsi kwa upande wa kuajiri wafanyikazi. Ni vigumu kupata kazi ikiwa hujui mtu mkubwa katika shirika linalohusika au uzunguke mbuyu. Matokeo ni kuajiri wafanyikazi wasiohitimu na wasiohitimu na wasiowajibika kazini.

Vyeo na madaraka katika baadhi ya mashirika hutolewa kwa njia ya mapendeleo na ufisadi. Kwa hivyo, wafanyikazi wenye biddi hufa moyo kwa sababu hawasaidiwi ipasavyo. Badala yake wale wasioleta bidii hupandishwa vyeo na kuwaacha palepale.

Hata hivyo, mbio za sakafuni huishaia ukingoni. Serikali imetangaza vita dhidi ya ufisadi. Tayari tume kadhaa zimeteuliwa kuchunguza visa vya ufisadi uliotekelezwa hapo mbeleni. Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya Kuchunguzavisa vya ufisadi uliotekelezwa hapo mbeleni. Mojawapo ya tume hizo ni Tume ya kuchunguza Kashfa ya “Goldenberg” ambapo pesa za umma (mabilioni ya shilingi) ziliporwa na mashirika na watu binafsi kwa njia siziso halali. Watakaopatikana na hatia ya kushiriki ufisadi huo watahitajika kurudisha pesa hizo.

Serikali pia imeunda kamati ya kupikea malalamiko kutoka kwa wananchi waliohasiriwa na mawakili walaghai ambao hupokea ridhaa kwa niaba ya wateja wao na kukosa wakalipa, au wakilipwa kuwatetea mahakamani wanakwepa jukumu hilo ilhali wamekwishalipwa. Ni matumaini yetu kuwa ulaghai huu utaangamizwa kabisa kwani hakuna refu lisilokuwa na ncha.

 

Maswali

1. Eleza aina nne za ufisadi zilizotajwa katika kifungu ulichosoma

2. Kulingana na kifungu ulichosoma, ufisadi umeathiri nchi yetu kwa njia gani?

3. Serikali inafanya jitihada gani ili kukomesha ufisadi?

4. Kwa maoni yako, unafikiri ufisadi husababishwa na nini?

5. Toa msamiati mwingine wenye maana sawa na rushwa

6. Eleza mana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumiwa kifunguni;

(a)
Majukumu  

(b) Kashfa

(c) Shamiri

(d) wakilia ngoa  

(e) Waliohasiriwa
 

(f) Kita mizizi  

 

6. Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali

Aibu kubwa ya taifa kushindwa kukabiliana na tatizo sugu la ajali za barabarani bado inaendelea. Wahusika katika sekta ya uchukuzi na mawasiliano licha ya matumizi ya vidhibiti mwendo na kanda za usalama. Ajali za barabarani zinaangamiza idadi kubwa ya watu kila mwaka, wakiwemo viongozi na watu mashuhuri.

Miongoni mwa sababu ambazo zinaleta maafa barabarani ni pamoja na uendeshaji kasi kupita inavyotakikana, yaani kukiuka masharti yaliyowekwa na wizara ya uchukuzi na mawasiliano. Madereva wengi hung’oa vithibiti mwendo vilivyowekwa hawarekebishi mikanda ya usalama, wala hawa peleki magari yao kwa ukaguzi mara kwa mara kama inavyopaswa kutekeleza kanuni zilizowekwa kwa hivyo hutegemea hongo kuwa barabarani. Fauka ya hao, madereva wa malori na matrela mara nyingi huendesha magari hayo wakiwa walevi. Dawa za kulevya kama vile miraa na bangi, hutumiwa sana na watu hawa, na matokeo yake huwa ajali mbaya.

Hata hivyo, lawama haiwezi kuelekezewa madereva pekee. Ukiangazia barabara nchini utapata kuwa barabara nchini Kenya haziko katika hali nzuri . Zile za lami zimekuwa na mashimo makubwa ambapo mvua ikinyesha hufanya vidimbi mithili ya machimbo ya madini yaliyojaa maji baada ya kuachwa wazi. Na zile barabara zisizokuwa za lami zimeharibika kiasi kwamba ni vigumu kuzitofautisha na njia za ng’ombe kwenye maeneo kame.Kinachohitajika ni serikali kuzifanyia ukarabati ili kuzirudisha katika kiwango ambacho zitaweza kufaa tena.

Wananchi pia inafaa waelimishwe ili wasikubali kuingia kwenye magari ambayo tayari yamejaaa kupita kiasi. Hili litawasaidia wananchi wenyewe kudumisha usalama wao barabarani. Pia inafaa watambue ya kwamba wana jukumu la kuwaarifu walinda usalama endapo dereva anaendesha kwa kasi sana kuliko ile ya kilomita 80 kwa saa iliyokubaliwa.

Inafahamika kuwa maafisa wa uslama ndio wafisadi zaidi, hivyo basi huchangia katika kuongeza idadi ya vifo barabarani. Katika vita dhidi ya ufisadi na ajali za barabarni, ni mwananchi mwenyewe ambaye alawezesha kukomesha hali hii. Kwa mfano, afisa wa usalama akipatikana akichukua hongo, yeye pamoja na yule aliyetoa hongo wapelekwe kwenye vituo vya kukabiliana na ufisadi na wachukuliwe hatua kali, matatizo haya yataisha.

Lakini kabla kufika hapo, ni muhimu kumhamasisha mwananchi kuhusu haki zake na namna ya kukabiliana na suala hili la ufisadi. Hali hii inatuonyesha kwamba mipango maalum inapaswa kufanywa na serikali ili kuwaelimisha wananchi kama hatua ya kwanza ya kukabiliana na ufisadi hatimaye izilainishe sekta zote wala si ya uchukuzi na mawasiliano pekee.

 

Maswali

1. (a) Mbali na ajali za barabarani, taja, tatizo lingine sugu ambalo linakumba nchi ya Kenya

(b) Ajali za barabarani zinasababishwa na nini?

  (c) Mwandishi anapendekeza hatua zipi zichukuliwe na serikali ili suluhisho la kudumu

lipatikane?  

(d) Taja hatua ambazo serikali imechukua ili kuimarisha uchukuzi  

(e) Ni kitu gani ambacho kinaonyesha kuwa serikali imeshindwa kukabiliana na ajali

barabarani?  

(f) Eleza maana ya maneno haya:-

(i) Tatizo sugu.

(ii) Vithibiti mwendo.

(iii) Machimbo.

(iv) Ukarabati.

(v) Hongo.

(vi) Kuhamasisha..

 

7.   Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali

Nchini Kenya, pamoja na kuwa mwanamke amepewa hadhi kubwa ikilinganishwa na hapo awali, kumetokea visa vingi vya unyanyasajiwa wanawake. Visa hivi haviwakati wengi maini, bali ni vyombo vya kuwazindua viongozi kuona kwamba hali haijafika kiwango cha kuridhisha. Visa vya ubakaji wa watoto wa kike na wazee, na wakati mwingine baba zao, vimetokea katika miaka ya hivi karibuni. Isitoshe, akina mama wengi wamekuwa wahasiriwa wa mivua ya makonde kutoka kwa waume zao, hata kwa makosa madogo madogo. Hivi majuzi mmoja wa wanawake hawa, ambao maisha kwao ni shairi tu, alichomwa vibaya na mumewe, kisa na maanaamejitia kujua kuwa kuna siku ya wapenzi, yaani Valentine day. Mwanamke huyu, baada ya kutoa mashambani kuja kujumuika na mumewe kusherehekea siku ya wapenzi, alipata sherehe za kuchoma moto huku mumewe akilalamika kuingiliwa uhuruwake. Mama huyu bado anauguza majeraha ya mwili na moyo!

Mwanamke aliyesoma na kupewa fursa ya kufanya kazi na ajira ofisini naye amekabiliwa na changamoto nyingi. Huyu lazima atekeleze majukumu yake kama mama, mke na mfayikazi. Wengi wa wanawake wanaofanya kazi mjini hulalamika wanafanya kazi maradufu ya wanaume. Mwanamke kama huyu, kama alivyolalamika mmoja wao ambaye ni afisa wa utawala wa mikoa, huanza siku yake alfajiri na mapema kuitayarishia familia staftahi, kisha kuelekea ofisisni ambapo anakabiliwa na migogoro mingi ya kusuluhisha. Arejeapo nyumbani jioni, hali huwa hiyo hiyo, kutayarisha chajio, kushughulikia kazi za shule za watoto na kuichangamsha familia. Maisha yake huwa hivyo, siku nenda siku rudi. Utashangaa mja huyu atayabeba mangapi?

Hali huwa mbaya zaidi kwa wanawake ambao wameingia siasa. Hawa mikasa yao haihesabiki. Mara watupiwe mabezo ya kila aina na wanasiasa wenzao, mara washutumiwe na kutiwa midomoni na wanajamii kwa kuonekana wakichapa kazi na kuwa na uhusiano wa karibu na wazalendo wenzao wa kiume. Maisha yake hupigwa darubini hata nyakati ambazo hayahitaji kuangazwa.

Mwanamke amekuwa kinyago cha kufanyiwa mzaha. Juzi karibu mbingu zianguke alipojitokeza mwana vitimbi mmoja aliyejitia kufanyia utani yasiyohitaji. Alimwasiri mwanamke kama aliyechangia kukosewa heshima kwake kwa kule kutamani kufanywa hivyo. Ingawa wanawake walimshinikiza mhusika huyu kuomba msamaha, upayukaji wake haupaswi kuchukuliwa kama mzaha. Ni ishara ya hisia ya ndani za watu wengi kuhusu mwanamke; kwamba ingawa wakenya wamejitahidi kupigania haki za wanawake; baadhi yetu bado wana zile fikira za kijadi kuhusu wanawake.

Uchumi wa nchi kamwe hauwezi kuendelea bila kumhusisha kila mtu. Nchini humu, baada ya kutambua haya, mwanamke amepewa nyadhifa mbalimbali katika serikali. Ingawa kuna baadhi ya wanawake waliohusika na kashfa mbalimbali za kifisadi, Kuna wale ambao wametumia nyadhifa zao kuhifadhi nchi. Mmoja wa wanawake amejaribu kwa jino na ukucha kuyalinda mazingira dhidi ya mapapa. Nani asiyekumbuka matusi na mabezo aliyopata mwanamke huyu anayejitoa mhanga kuikinga sehemu Fulani ya burudani dhidi ya kunyakuliwa na wanaostahili? Hakuyajutia yaliyompata. Aliowatisha walijaribu kummeza mzimamzima lakini mwishowe walisalimu amri na kuliacha eneo hilo. Hiki kilikuwa kitendo cha ujasiri na uzalendo mkubwa. Matunda yake yamewafaidi wengi, vijana kwa wazee. Kila mwisho wa wiki huwaona watu wakimiminika kwenye eneo hili kujipumbaza. Hii si fahari kwake tu, bali kwa nchi kwa jumla. Wale waliompinga na kumwita punguani wakati huo wamebaki kuinamisha nyuso tu; bila shaka wamefunzwa mengi.

Wanawake sasa wana haki ya kumiliki mali mathalani shamba. Kutokana na hili tumeshuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji wa chakula mashambani na kwa hivyo kupunguza njaa na umaskini.

Biashara ndogondogo zinazoendelezwa sokoni na mitaani, kwa kiasi kikubwa, huhusisha wanawake. Biashara hizi huchangia pakubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi kwani hutoa ajira ya kibinafsi kwa maelfu ya watu. Ushuru na leseni zinazokatiwa biashara hizi huongezea serikali pato la ndani.

Mgala muuwe na haki umpe. Ni ukweli kwamba tumekuwa na visa vya hapa na pale vya ukiukaji wa haki za wanawake. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba nchi hii imejitahidi mno kuendelea kumkwamua mwanamke kwayo. Hata mashirika ambayo hapo awali hayakupenda kuwaajiri wanawake, sasa yanawapa nafasi sawa na wanaume. Vyuo vikuu vya kibinafsi vimeanzishwa kuwasajili wanawake. Jijini humu, mna chuo kikuu cha sayansi cha wanawake. Aidha kumeanzishwa kituo (shule) cha kuwasajili wasichana kutoka familia maskini kujiunga na kidato cha kwanza. Wasichana hawa watapata wadhamini kutoka mashrika na watu mbalimbali ili kujiendeleza kimasomo.

Kumheshimu mwanamke ni miongoni mwa haki za kibinadamu ambazo shart zitekelezwe. Hata hivyo, wanawake wakumbuke kwamba hata wanapopuliza siwa kuhusu pupewa haki, lazima wao pia wawajibike. Wao ndio walimu wa kwanza wa wanao; ikiwa basi wataonekana kwenye vyombo vya habari wakining’inia juu ya magari ya wachunga magereza kwa kuzitafutia pesa za mayatima maumizi bora, watakuwa wanapotosha watoto wao. Wawe watu wa vitendo zaidi ya upayukaji.

 

Maswali

a) Kwa mujibu wa taarifa, ni mambo yapi yanayoonyesha ukiukaji wa haki za wanawake  

b) Fafanua jinsi mwanamke aliyesoma huteseka maradufu zaidi ya mwanamme

c) Ni faida gani ambazo zimepatikana kutokana na wanawake kupigania haki zao?    

d) Hatimaye wanawake wanahimizwa kufanya nini?

 

e) Eleza maana ya msamiati ufuatao jinsi ulivyotumiwa katika nakala  

  Kinyago…

  Mabezo

f) Andika mfano wa mbalagha na uhuishi uliotumiwa katika makala haya

i) Mbalagha…………

ii) Uhuishi…………  

 

8. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali:-

Uundaji wa istilahi – hasa za lugha ya Kiswahili ni shughuli nyeti na nzito hivi

kwamba, haipaswi kupapiwa na mtu yeyote. Hii ni shughuli inayohitaji umakinifu zaidi kwa wanaoshiriki katika mchakato wa uundaji istilahi za kutufaa katika mawasiliano na kukuza Kiswahili kwa jumla. Ufanisi wa watu binafsi, vyombo vya habari kama vile Shirika la Habari la Kenya (KBC), Taifa Leo na mashirika mengineyo katika ukuzaji wa lugha hutegemea mno sera na utayarishaji wa serikali katika kugharamia shughuli hii. Aidha, shughuli za kukuza lugha hukwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha pamoja na sera maalum ya serikali kuhusu lugha.

Hata hivyo, katika kuyakwepa matatizo haya, pamekuwepo na hatua za kimataifa za kujaribu kusawazisha shughuli ya uundaji wa maneno. Hatua hii ilichochea kubuniwa kwa shirikisho la kimataifa la vyama vya usanifishaji istilahi mnamo 1936. Lengo la kitengo hiki lilikuwa ni kufafanua msingi madhubuti ya uundaji wa istilahi duniani. Kwa hakika, shirikisho hilo limesaidia mno katika kuweka misingi ya shughuli za ukuzaji wa istilahi. Misingi hiyo ni ya jumla na haihusu taaluma yoyote mahususi. Katika makala hii, tunapiga darubini baadhi ya misingi hiyo pamoja na mapendekezo yake.

Mosi, uundaji istilahi unafaa uanzie kwenye dhana na wala sio neno. Hii ina maana kwamba, kwanza pawepo na dhana au hali ambayo inahitaji itafutiwe neno au istilahi ya kuielezea. Inasikitisha sana kwamba pana wataalamu ambao wanaukaidi au kuukiuka msingi huu. Wanataaluma hawa hufanya mambo kinyume kwa kujibunia maneno yao na kuyahifadhi kwenye mikoba yao – halafu wakasubiri dhana izuke ndiposa waipachike istilahi yao. Pili, dhana zinabuniwa au kutolea istilahi au maneo ni muhimu zielezwe kwa ukamilifu na uwazi. Istilahi zinazoundwa zinafaa ziwe fupi iwezekanavyo na ziwe na uwezo wa kuelezea dhana kwa njia inayoeleweka bila utata. Tatu, maneno yanayoundwa sharti yawe na uhusiano wa aina fulani na dhana zinazowakilishwa na maneno hayo.

Uhusiano huo unaweza kuwa ama ni wa kimaumbile au wa kiutendaji. kwa mfano, Mzee Sheikh Nanhany wa Mombasa alipobuni istilahi ‘uka’ kwa maana ya ‘ray’. Neno hili latokana na kupambauka au (kupambazuka kwa lafudhi ya kiamu. Neno ‘image’ ni jazanda kwa Kiswahili. ‘Mirage’ kwa Kiswahili ni ‘mangati’ (kutoka kwa mang’aanti) – yaani kung’aa kwa nchi. Mtaalamu mwingine aliyewazia uendajikazi wa kifaa na kubuni istilahi inayokubalika mpaka sasa ni Prof. Rocha Chimerah ambaye alibuni istilahi ‘tarakilishi’. Pengine Prof. Chimerah alifikiria kazi ni kifaa husika na kuunda neno la Kiswahili linaloakisi kazi hiyo. Tunajua kwamba kompyuta hufanya kazi inayohusu tarakimu kwa haraka kama umeme. Labda Chimerah ameegemea sifa hii kuibuka na istilahi hii.

Maneno mengine ambayo yamebuniwa kufuatana na msingi huu ni ya Mzee Nabhany-mathalan ‘barua pepe’ (e-mail), na wavuti (website). Tukiegemea maumbile, neno ‘kifaru’ lina maana ya vita ilihali tuna zana ya vita iliyopewa jina hilo kwa sababu ya labda kuwa na maumbile sawa na kifarumnyama. Nne, istilahi zinaweza kukopwa kutoka lugha nyingine. Yamkini hakuna lugha hata moja ulimwenguni-zikiwemo lugha duniani kama vile kiingereza zinazoweza kujitosheleza. Takriban asilimia 80 ya maneno katika kiingereza ni ya kukopwa. Kwa hivyo, lugha ya Kiswahili inapokopa, hali hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa ni lugha dhaifu.

Hata hivyo, istilahi zinazokopwa zi-nafaa zichukuliwe zilivyo katika umbo lao asili. Umbo hili linaweza kufanyiwa marekebisho machache tu, kulingana na sarufi na matumizi ya lugha kopaji. Mifano ya istilahi kama hizi ni ‘televisheni’ (television), kopmpyuta (computer), kioski (kutokana na jina ‘kiosk’ la Kijerumani) na redio (radio), Tano, pale istilahi haiwezi kukopwa, lugha husika ijaribu kubuni msamiati ufaao, kufanya hivyo ni kuhakikisha kwamba, lugha inastawi. Lakini tahadhari inapaswa kuchukuliwa hivi kwamba, Kiswahili kisikope maneno kiasi cha kupoteza upekee wake. Mwisho, uundaji wa istilahi uzingatie mofolojia ya kawaida ya lugha. Istilahi zinazoundwa kwa kuzingatia mofolojia huwa rahisi kuiua maneno yenye uhusiano wa istilahi asili kwa njia ya mnyambuliko.

 

Maswali

(i) Taja mambo ambayo huchnagia ukuaji na ufanisi wa jumla wa lugha ya Kiswahili  

(ii) “Lugha ya Kiswahili ni dhaifu na isiyotosheleza” Je, mwandishi wa makala haya

ana msimamo upi kuhusu kauli hii?

(iii) Tahadhari zipi zinazofaa kuchukuliwa kabla ya kukopa istilahi kutoka lugha zingine?  

(iv) Yape makala haya anwani mwafaka

(v) Eleza maana ya maneno yafuatayo:

(a) Dhana-  

(b) Takribani –  

(c) Istilahi – .

(d) Mofolojia –…  .

 

9.  Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali:-

Kitabu kinaeleza Mungu kamuumba mwanamke kutokana na ubavu tu wa mwanamume. Na hapa bila shaka ndipo linapojisalimishia shina lisilokuwa na mzizi thabiti la ubinafsi wa kiume – mwanamume akijijadilia kimoyomoyo. Ikiwa huyu mwanamke alitokana na ubavu wangu, yeye awe nani kwangu? Hakuna shaka ni wangu, mali yangu. Kwa sababu hii, miaka nenda miaka rudi mwanamke amekuwa akiugua na kuguna chini ya uonevu wa mwanamume.

Swala la kitabu kumleta duniani mwanamke kupitia ubavu wa mwanamume laweza kueleweka katika muktadha wa kile ambacho kimekuja kujulikana kama taasubi ya kiume. Na ili tuelewane barabara kuhusu maoni haya, tujisitishe kidogo katika kunusa tumbako huku tukijiuliza: ni nani au ni kina nani walihusika katika kubuni au kuandika hadithi ya asili ya mwanamke kitabuni? Ni kawaida ya binadamu kutazama na kueleza jambo kibinafsi. Asili ya mwanamke ilivyoelezwa kitabuni katika mkururo wa fikra hii yaweza kutambulikana kama uzushi tu.

Kiutamaduni, hasa wa Kiafrika, huku akiwa yuakua, mtoto wa kike husombezewa kasumba ya mawazo akilini, na kwa bahati mbaya sana, aghalabu na mamake au nyanyake, kuhusu namna anavyotarajiwa kutabasamu, kujinyenyekeza, na jumla kujidunisha mbele ya mvulana. Ni mwiko kwake
kudhihirisha tabia za kimabavu, sitaji kujitetea, ili asije akatiwa mdomoni mitaani! Msichana atacharazwa na wazazi wake kwa ujasiri licha ya kuthubutu kupigana na mvulana. Na hapo ndipo ilipojificha siri ya kuwa anapoolewa na akosane na mumewe, daima yeye hutolewa makosa na kupatikana na hatia mbele ya wazee.

Wavulana kwa upande wao ni wanaume na lazima afanye mambo kiume. Si ajabu kuwa kinyume cha yale yanayowafika wasichana, wavulana wengi huonyeshwa mbovu na baba zao kwa sababu wamepigwa na wenzao. Ni vibaya baba kusikia mtoto (mvulana) wake amepigwa.

Nyumbani msichana hutarajiwa kujilindia heshima kimwili hasa kwa kuhifadhi ubikira mpaka aolewe. Anapotembea na wanaume huitwa Malaya. Ni ajabu kuwa hakuna bikira wala Malaya mwanaume. Mvulana ambaye hajajuana kimwili na mwanamke kabla ya ndoa huchukuliwa kuwa zuzu; ilhali anayetembea ovyo na wanawake ndiye dume.

Fauka ya hayo, inasikitisha kabisa kuwa mwanamke hana mahali pa kutua kikamilifu duniani. Kabla hajaolewa nyumbani, huchukuliwa kuwa mpita njia tu. Na anapoolewa ni poa kaolewa. Isitoshe mwanamke huolewa, haoi wala yeye na mume hawaoani. Mwanamke mahali pake ni jikoni pia anaonekana tu; ni hatia kwake kujaribu kusikika.

Mkutano kuhusu mwongo wa wanawake uliofanyika miaka miwili iliyopita jijini Nairobi ilinuiwa kupalilia vizuri mwamko juu ya ukweli kuwa binadamu ni binadamu na hakuna haja ya wao kubaguana. Tofauti za kimaumbile haziwezi kuwa hoja. Tusiupigie makelele ubaguzi wa rangi huko Afrika kusini ilhali kwetu tuna ubaguzi wa kimaumbile. Tusipozingatia ushauri huu daima tutakuwa kwenye kile kinaya cha kuchekwa katika muktadha wa methali kuwa nyani haoni ngokoye.

Ni kweli kosa lilifanyika tangu awali ambapo kufumba na kufumbua, mwanamke akapigwa jeki na kuachwa akilewalewa katika hali ambayo hangeweza kujitetea hivyo basi akachukuliwa kuwa kiumbe duni. Lakini haidhuru, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kinachohitajika ni wanawake kuwa na nia na msimamo imara. Ni lazima wajifunge kibwebwe na kujitoa mhanga na kupambana dhidi ya taasubi ya kiume.

 

Maswali

 

(a) Andika kichwa kinachofaa kutokana na taarifa uliyoisoma  

(b) Taasubi ya kiume ilianzaje?

(c) Katika utamaduni wa mwafrika ni kasumba gani anayosombezewa mtoto wa kike anapokua?

(d) “Wavulana walidekezwa na utamaduni”. Eleza

(e) Taja kwa ufupi mambo muhimu yaliyoshughulikiwa katika mkutano wa mwongo wa

wanawake mjini Nairobi

(f) Eleza maana ya semi zifuatazo kama zilivyotumiwa katika taarifa uliyosoma:-  

  (i) Nyani haoni ngokoye  .

  (ii) Akatiwa midomoni  

  (iii) Huonyeshwa mbovu  

  (iv) Wajifunge kibwebwe  

  (v) Yaliyopita si ndwele ganga yajayo  

 

10. Soma taarifa hii kisha ujibu maswali

Asifuye mvua imemnyea. Huu ni msemo wenye hakika isiopingika, na kutilia shaka ni sawa na kudai jua linaweza kubadilika na kuchomozea upande wa magharibi badala ya mashariki. Huu ndio ukweli uliodhihirika juzi katika vyombo vyetu vya magazeti.

Lisemwalo lipo, na kama halipo li njiani. Waama, pafukapo moshi pana moto. Mwanafunzi mmoja wa kike kwa jina P.N. katika chuo kikuu kimojawapo nchini alishangaza umma wa Kenya na ulimwengu kwa jumla alipodai kuwaambukiza wanafunzi wenzake wa kiume mia moja na ishirini na wanne virusi vya Ukimwi.

Kisa na maana? Aliambukizwa Ukimwi na mwanafunzi mwenzake aliyekuwa akifanya majaribio ya ualimu katika shule yao ya upili. Baada ya kushawishika sana alijuana naye kimwili, na matokeo yakawa kifo ambacho sasa alikuwa anawagawia wenzake.

Kisa kama hiki kinachangia kueleza kina kirefu cha kutamauka na upweke ambao maisha ya waja wengi yameingia kiasi cha kuwaacha wanyama ijapo wanaenda kwa miguu miwili bado. Katika mojawapo ya mafunzo ya kidini ambayo Padre alinifunza mimi na wanafunzi wenzangu, tuliambiwa kisasi ni chake Mola, sisi waja wetu ni kushukuru tu. Mbona basi mwanafunzi kama huyu kutaka kulipiza?

Ima fa ima, na waswahili husema, “mlaumu nunda na kuku pia”. Huyu mwanafunzi hawezi kuachiwa atende alivyotenda. Aliyekula naye raha alikuwa mtu aliyefahamika vizuri sana kwake. Isitoshe, huenda wakati huo alikosana na mama na baba kulala nje. Huenda alikosana na ndugu zake kwa kuepa nyumbani usiku wa manane kwenda kumwona huyu kalameni. Huenda alikosana na mwalimu wake kwa sababu kiburi kilianza kuingia. Kwa vyovyote vile, alikula raha na hastahili kuwaadhibu watu wasio na hatia kufidia makosa yake. Je, kama yeye na huyo jamaa wasingekuwa na Ukimwi, raha kiasi gani wangezila hadi leo?

Jamii na watu wote kwa jumla hawana budi basi kulaani vitendo vya P.N. vya kuambukiza wanafunzi wenzake virusi huku akijua. Hili ni kosa ambalo linastahili adhabu ya kifo. Dawa ya moto ni moto ni adhabu inastahili kuchukuliwa haraka ili P.N. ambaye tayari amekiri hatia, atiwe nguvuni na adhabu itolewe.

Barua ya P.N. inafafanua jambo jingine sugu. Kwamba kiwango cha maadili katika vyuo vyetu kimezorota kiasi cha kufanyiana unyama usiosemeka. Vijana wengi siku hizi wanashiriki tendo la ndoa bila haya. Huu upotofu wa maadili katika jamii wapaswa kushutumiwa na wote. P.N. hana sababu yoyote ya kibinadamu, kidini au kitu chochote kile kudai haki kwa uovu huo wake.

 

Maswali

1.Taja kichwa kwa makala haya

2. Katika aya mbili za kwanza, mwandishi anamlaumu mwanafunzi kwa kosa gani? Eleza chanzo cha tabia za P.N

4. Mwandishi wa taarifa hii anataka P.N achukuliwe hatua gani? Kwa nini?

5. Barua ya P.N. bila shaka imeonyesha uvumbuzi mpya. Utaje  

6. Eleza maana ya vifungu hivi kama vilivyotumiwa katika taarifa:  

(a) Kina kirefu cha kutamauka

(b) Ima fa ima

(c) Kufidia makosa yake

 

11. Soma taarifa hii kisha ujibu maswali

CHIMBUKO LA USHAIRI

Ushairi ni fani kongwe kama mwanadamu mwenyewe alivyo mkongwe duniani. Na mashairi yamekuwepo kitambo sana hata kabla ya lugha ya Kiswahili bado haijanawiri na kushamiri kama ilivyo hivi leo. Ndipo tunasikia kuna mashiri ya kipemba, mashairi ya kimvita, mashairi ya kivumba, mashairi ya kipate, mashairi ya kiyunani, ya kirumi na kadhalika,. Almradi kila jamii na kila kabila lilikuwa na mashairi yake.

Katika utafiti na kongomano zao, wataalam wa arudhi za Kiswahili asili wamechambua na kufafanua kwamba mashairi ya Kiswahili asili yake ni nyimbo za jadi zilizokuwa zikiimbwa na manju, wangoi au waimbaji stadi wa tangu na tangu walipojumuika katika matukio na hafla mbalimbali kama za jando, arusi, matanga, ngoma na shangwe zao za maishani.

Nyimbo hizi zilitumiwa na watangulizi wetu, kidhamira hazikuhitalafiana hata kidogo na mashairi ya Kiswahili tunayohimiza wakati huu. Farka iko katika lugha na umbo kwani kila jamii ilitumia lugha yake na lahaja ya mazingira yake. Na kwa upande wa umbo, tungo hizo za awali kabisa hazikuwa na sanaa kwa maana ya ushauri tunauona leo. Bali tungo hizo zilijengeka katika nguzo mbili kuu. Kwanza ni uzito wa mawazo maadilifu ambayo yalitaamaniwa sana. Na pili ni mizani ya sauti ya manju kulingana na lahani, pumzi zake pamoja na madoido katika uimbaji ambao ulikuwa burudani naathari katika noyo za wasikilizaji wake.

Kwa kifupi ni kwamba, nyimbo hizo ziliuhifaid umma kwa njia mbili, mawaidha kwa mapana na taathira au jadhba kutokana na sauti tamu ya manju.

Kama utakubalika, basi huo ndio ushairi wa awali kabisa ullioambatana na nyimbo zetu za kienyeji. Kila kabila katika nchi zetu lilikuwa na ushauri wake au nyimbo zake zenye undani uliolenga sababu maalum na tukio maalum katika jamii.

Nyimbo kama hizo kwa jina la sasa tunaweza kuita mashairi ndizo zile zilizoitwa ‘mwali’ na wakamba; gichandi kwa ‘wakikuyu’; ‘gigia gi sigele’ kwa waluo na ‘wagashe’ kwa wasukuma zilikuwa na undani wa kipekee tena uliodidimia ambao si bure kutolewa hadharani.

Aina za mashairi ya watu wa mwambao ni kama lelemama, misemele, gungu, nyiso, kongozi n.k.

(Walla Bin Walla – Malenga wa Ziwa Kuu , E.A.E.P)

1. Ni nini haswa chimbuko la ushairi?

2. Kulingana na kifungu hiki, ni nini umuhimu wa ushairi ?

3. Ni maswala gani yaliyowapendeza wasikilizaji wa tungo hizo za zama ?  

4. Tofauti kati ya nyimbo za zama na ushairi wa leo upo kwenye vipengele gani viwili ?

5. Kifungu : ‘haijanawiri na kushamiri’ ina maana gani katika lugha nyepesi ?

6. Eleza maana ya :  

(a) Kongamano …

(b) Jadhiba

(c) Farka

   (d) Awali..


12. Soma taarifa hii kisha ujibu maswali

Chamkosi alipiga goti huku machozi yakimdondoka njia nne nne. Mbele yake, palikuwa na makaburi mawili. Waliokuwa wamelala mle hawakuwa na habari juu ya kihoro na simanzi ya aliyepiga magoti pale. La kwanza, lilikuwa kongwe kiasi na lilikuwa limemea vichaka na magugu. La pili lilionyesha upya kwani shada za maua zilizowekwa na waombolezaji zilikuwa bado kukauka. La kwanza, ndimo babake mzazi alipolala. Nalo la pili, ndimo mamake alimolazwa kiasi cha siku mbili zilizopita.

Kwa Chamkosi, maisha hayakuwa na maana tena. Alikuwa mwanafunzi wa miaka kumi na miwili. Hakuwa amehitimu kujitegemea na kukimu mahitaji yake. Aliokuwa akiwategemea sasa wamemwacha akiwa yatima. Hakuna yeyote ambaye angejaza pengo la wazazi wake wawili kwa kipindi cha mwaka mmoja. Haya yalikuwa kama donda sugu lisilopona.

Kwa sasa, Chamkosi anayakumbuka mengi. Anakumbuka maisha ya babake. Alikuwa jibaba nene, zito lenye sura jamala na sifa nzuri. Baba mtu alikuwa na chake na alijiweza kiuchumi. Wengi pale mjini walimheshimu na kumstahi kutokana na uwezo wake wa kiuchumi. alitunza familia yake vizuri. Chamkosi hakumbuki siku moja aliyokosa chochote alichohitaji kutoka kwa babake. Alikuwa na bidii kazini mwake pia.

Walakini, kama mja asiyekamilika, baba mtu alikuwa na dosari moja. Aliyapenda maisha ya anasa na kufukuzia wasichana wadogo pale mtaani. Mamake Chamkosi aliyajua haya. Alijaribu kuzozana na mumewe ili aachane na tiabia hizi lakini kila akitaka ushauri, mama mtu alikemewa na kufokewa kuwa aache upuzi wa wanawake. Akafikia kufyata ulimi na kumwachia Mungu aongoze maisha ya bwanake.

Hata hivyo hakuna marefu yasiyo na kikomo. Baada ya kuponda raha na vimada si haba, baba mtu alianza kuugua. Maradhi yake yakawa ni msururu. Mara, alipata mafua yasiyopona, mara kuendesha, mara maradhi ya ngozi. Haya yalimtia wasiwasi. Baada ya kukaguliwa na daktari, alipatikana kuwa ameumwa na mbuzi. Hakuamini haya. Baba aliyekuwa bashasha na mcheshi aliingiwa na upweke na kutotaka kutangamana na yeyote hata jamaa zake.

Waliosema kuwa hakuna msiba usiokuwa na mwenzake, hawakukosea. Maradhi ya baba mtu yaliifilisi jamaa huku waking’ang’ania kumtafutia tiba. Wakaenda kwa waganga si haba. Waganga nao wakafaidi tamu.

Muda si mrefu, mama mtu naye akaanza kuugua. Baada ya uchunguzi, alipatikana kuwa na maradhi yayo hayo ya bwanake. Ikawa ni kama mji umelogwa. Baada ya muda mfupi baba mtu aliaga dunia, mama naye hakukawia. Naye akasalimu amri na kumfuata bwanake kaburini. Familia ikawa kama inaangamia. Chamkosi kijana mdogo akaachwa pweke.

Kama kawaida, mja hakosi neno. Wengi walisikika wakisema hili na lile kuhusu vifo hivi. Wengi walieneza uvumi. Lakini, Chamkosi alijua ukweli wa vifo vya wazazi wake.

Sasa hapa alipo aliyatambulia macho makaburi ya wazazi wake, anasononeka. Anaomboleza zaidi kifo cha mamake ambaye alimwona hana hatia na hakupaswa kufa kwa maradhi yale. Anaukumbuka vizuri wema wa mamake usio na kifani. anakumbuka alivyojitunza kama mke na mzazi.

Anakumbuka jinsi mamake alivyomshughulikia babake katika siku zake za mwisho licha ya baba mtu kuungama maisha yake maovu. Chamkosi alishindwa kujua kwa nini mamake akawa msamehevu kiasi hicho. Hakukosa kukumbuka wasia wa mama yake. Haya yalimfariji. Faraja hizi zilimpa nguvu mpya za kuyakabili maisha.

Chamkosi aliwaza juu ya maisha yake. Akaona kuwa, kama yatima atawategemea wafadhili miongoni mwa jamaa na marafiki wenye huruma iwapo wapo. Aliwaza jinsi anasa za babake zilivyowaathiri watu wengi.Alitambua kuwa Ukimwi haumwathiri aliyeupata tu, bali na wengine wengi. Kweli, mtego wa Panya huingia waliokuwemo na wasiokuwemo. Lakini akiwatazama watu, hakuelewa kwa nini walidhamiria kuishi ujingani. Aliwaona baadhi ya vimada wa babake wakishikana viuno na vijana wadogo. Akawasikitikia. Akabaki na swali kwa nini watu wengine wanafikiria kuwa virusi hivi haviwezi kuwapata. Kwani wanafikiria kuwa vinabagua na kuwa wao hawahatarishi maisha yao? Alishindwa kufahamu watu watabadili vipi mienendo yao miovu na waweze kukabili janga hili lini?

Kwa wakati huu, Chamkosi alikata shauri kusomea Taaluma ya Uelekezi na Ushauri kutokana na vifo vya wazazi wake. Alitaka kupata ujuzi utakaomwezesha kuwashauri na kuwaelekeza vijana wenzake ambao wanahatarisha maisha yao. Kama mshauri, alinuia kuhamasisha na kuzindua jamii juu ya hatari za Ukimwi.

Alitaka kuhakikisha kuwa hatua zimechukuliwa na kila mtu katika jamii kukabili janga hili n kuliangamiza

Chamkosi aliomba dua fupi. Akainuka na kuondoka huku akiwa na faraja na matumaini moyoni kutokana na azimio lake lile.

 

(a) Toa kichwa mwafaka kwa makala haya

(b) Eleza madhara mawili ya ugonjwa sugu uliotajwa katika makala haya  

(c) Taja mifano ya tabia zinazoweza kumfanya mtu aathiriwe na ugonjwa wa Ukimwi

(d) Tofautisha tabia za baba na mama wa Chamkosi  

(e) Chamkosi baada ya kufikwa na madhila hayo yote aliamua kufanya nini? Toa maoni

 (f) Eleza maana ya:

(i) Tumbulia macho …………………………………………………………………………………………………

(ii) Ameumwa na mbuzi…………………………………………………………………………………………

 

 


13. Soma taarifa hii kisha ujibu maswali  

Licha ya kuwa na historia ya kiasi, maisha ya binadamu ni kioja kikubwa. Hebu jiulize jinsi uhai wako wewe mwenyewe ulivyoanza sembuse unavyoweza kupumua na kuishi siku nenda siku rudi.

Dini zimefahamisha kuwa sisi binadamu tumeumbwa na Mwenyezi Muumba. Hata hivyo muumba hutumia mume na mke kutuanzishia maisha yetu humu humu duniani. Uhai wa hapa duniani huanzia katika tumbo la mwanamke muda mfupi tu baada ya mume na mke kushirikiana katika tendo la kujamiana. Katika ngono hii yenye ufanisi, mbegu moja ya manii kutoka kwa mwanamume, hudunga na kujiingiza katika yai la mwanamke huku ikilirutubisha. Tangu hapo mtu huwa na mama akawa mjamzito. Hatua ya kwanza ya uhai!

Wanasayansi wametuthibitishia kuwa mbegu katika shahawa kutoka kwa mwanamume ina kromosomu ishirini na tatu (23) nalo yai la mwanamke lina idadi iyo hiyo ya kromosomu. Basi katika hatua ya kwanza ya uhai wake, binadamu ana kromosomu arubaini na sita (46).

Kromosomu hizo zote ndizo humfanya mtu kuwa mkamilifu kwa kukadiria mambo mbalimbali adhimu. Kwa mfano, kukadiria kama kiumbe kitakuwa cha kike au cha kiume, mtu mweupe au mtu mweusi, mwerevu au wa wakia chache, mwenye nywele za singa au za kipilipili, atakuwa na damu ya namna gani, michoro ya vidole vyake itakuwa vipi na hata utu wake utakuwa wa namna gani katika siku za usoni.

Elimu yote anayopata mtu kutoka kwa jamii na mazingira huweza tu kujenga juu ya yaliyokwisha kuanzilishwa na kromosomu katika yai lililorutubishwa tumboni.

Haihalisi kabisa kufikiria kwamba huwa katika hali ya ukupe. La hasha! Yeye hujitegemea kwa vyovyote na ana upekee wake. Hatangamani na mama yake. Roho yake humdunda mwenyewe na damu yake ambayo huenda ikawa tofauti kabisa na ya mama yake, humtembea na kumpiga mishipani mwake. Isitoshe, yeye si mojawapo katika viungo vya mwili wa mama yake vinavyomdhibiti katika himaya yake ndogo.

Amini usiamini, hapana binadamu hata mmoja ambaye amewahi kuwa sawa kimaumbile na mwingine na wala hatakuweko. Hata watoto pacha kutoka yai moja la mama hawawi sawa, lazima watofautiane. Si nadra kusikia mtu amepata ajali akahitaji msaada wa damu, na pakakosekana kabisa mtu hata mmoja kutoka jamaa yake wa kimwauni. Basi ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.

Maswali-

1. Ipe taarifa uliosoma anwani mwafaka

2. Mwandishi ana maana gani anaposema ‘ngono yenye ufanisi’?

3. Uchunguzi wa sayansi umekita mizizi imani gani ya kidini?

4. Taja majukumu yoyote matano yanayotekelezwa na kromosomu  

5. Katika makala, elimu kutoka kwa jamii na mazingira yaelekea kuwa bure ghali. Kwa nini?  

6. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika makala:-

   (i) huwa katika hali ya ukupe…

(ii) himaya

   (iii) hatangamani na mama yake

 

14.  Soma ufahamu ufuatao kisha ujibu maswali

Kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita, ulimwengu mzima uliathiriwa na masaibu ya kifua kikuu kwa kiwango cha kuogofya kiasi kwamba katika mwaka wa 1993, shirika la afya duniani (WHO) lilitangaza ugonjwa huu kuwa swala dharura la kimataifa.

Ongezeko kubwa la visa vya kifua kikuu lililotokana na kuchipuka kwa viini vinavyosababisha maradhi hatari ya Ukimwi na magonjwa yaliyohusiana na punde baadaye ilibainika kuwa bara la Afrika lilikuwa ndilo lililoathiriwa zaidi na Ukimwi pamoja na maradhi ya kifua kikuu. Hii ndiyo hali inayotawala sasa ulimwenguni. Afrika likiwa bara linaloongoza kwa wagonjwa walioambukizwa viini vya Ukimwi lilikuwa likishuhudia visa vya maradhi ya kifua kikuu.

Viini vya Ukimwi vinapunguza uwezo wa mwili wa mgonjwa kupigana na vijidudu vya maambukizi. Swala linalowafanya wagonjwa hawa kutodhibiti maambukizi ya magonjwa mbalimbali. Katika hali ya kawaida mwili wa mtu kama huyo unaweza kujikinga dhidi ya viini kama hivyo. Maambukizi kama haya kawaida hujitokeza kukiwa na nafasi duni ya kinga mwilini. Katika baadhi ya mataifa kama vile Kenya, maambukizi ya kifua kikuu hufanyika mapema katika umri mchanga maishani.

Kwa kawaida, viini hivyo huwa havisababishi ugonjwa wenyewe. Badala yake, kinga katika mwili wa aliyeambukizwa unaweza kusitiri maambukizi hayo bila mhusika kuwa mgonjwa kutokana na sababu mbalimbali. Viini hivyo baadaye vinaweza kuwa hai tena na kumfanya mgonjwa kukumbwa na ugonjwa. Swala hili kwa kawaida hujitokeza wakati mgonjwa anapoambukizwa virusi vya Ukimwi. Virusi hivyo pia huongeza hatari ya ugonjwa kujitokeza baada ya maambukizi au pengine kujitokeza tena baada ya mgonjwa kupokea tiba ya kwanza.

Kulingana na utafiti, inakadiriwa kwamba mmoja kati ya wagonjwa wawili au watu wenye virusi vya Ukimwi watapata kifua kikuu wakati mmoja katika maisha yao. Inakadiriwa kwamba karibu asilimia 50 hadi 60 ya wagonjwa wenye maradhi ya kifua kikuu nchini Kenya pia wameambukizwa viini vya Ukimwi. Kwa upande mwingine, maradhi ya kifua kikuu hujitokeza kama kawaida kwa wagonjwa wenye virusi vya ukimwi. Kwa hivyo, wakati wa kushughulikia wagonjwa ni lazima pia wafanyiwe uchunguzi wa kubaini ikiwa wameambukizwa kifua kikuu.

 

Maswali

 (a) Ipe taarifa uliyoisoma kichwa mwafaka  

 (b) Ni nini hasa kilichochangia kuongezeka sana kwa maradhi ya kifua kikuu?

 (c) Kwa kifupi, eleza ni kwa nini ugonjwa wa Ukimwi ni hatari mwilini  

 (d) Ukimwi na kifua kikuu una uhusiano mkubwa, eleza uhusiano huu kulingnana na

taarifa uliyoisoma

 (e) Andika urefu wa neno ‘Ukimwi”

 (f) Eleza mambo mawili ambayo yametokana na utafiti

  (g) Ni jambo lipi ambalo ni la kushangaza kuhusiana na kifua kikuu  

  (h) Andika maana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika kifungu hiki

(i) Kusitiri

(ii)Mwongo

(iii) Swala la dharura.

(iv)Viini
15.  Soma makala yafuatayo kisha kisha ujibu maswali:-

Waajiri wengi wanazilaumu taasisi za elimu kwa kukosa kutoa wafanya kazi wenye ujuzi tosha, hasa wa kiteknolojia za kisasa kama kutumia kompyuta kutenda kazi mbalimbali. Hali hii imekuwa ya kuhuzunisha sana.

Ujuzi wa kuweza kutumia Kompyuta unaweza kumfaa mwanafunzi hata anapokosa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu kwa vile anaweza kuendelea na elimu yake kupitia kwa elimu mtandao. Pia anaweza kufanya utafiti wa kina kupitia intaneti na kwa njia hii akaimarisha elimu yake.

Mojawapo ya njia ya kuimarisha elimu kuhusu maswala ya teknolojia ni kuanzishwa kwa mikakati mipya ya kufunza. Somo la Kompyuta laweza kuimarika mashuleni endapo kwanza walimu watahamasishwa juu ya faida za ujuzi huu.

Kwa kutumia Kompyuta kufunza, walimu wanaweza kufunza madarasa kadhaa katika kipindi kimoja bila kulazimika kuyahudhuria. Hii itapunguza kiwango cha kazi kwa walimu kwa vile watapata muda wa kufanya utafiti mpana. Aidha, watapata habari na ufahamu zaidi wa mambo kwa kutumia mitambo ya Kompyuta kutoka kwenye intaneti, kupitia tovuti.

Hata hivyo mipango hii inakabiliwa na changamoto kama vile bei za juu za mitambo na vifaa vya Kompyuta, ukosefu wa miundo msingi itakayowezesha utumiaji wa mitambo hii na ukosefu wa walimu waliohitimu somo la Kompyuta.

Pia, kuna tatizo la ukosefu wa nguvu za umeme hasa maeneo ya mashambani; vile vile, katika maeneo yaya haya, wanafunzi na wazazi wengi huvichukulia somo la Kompyuta kuwa gumu na linalofaa wakaazi na wanafunzi kutoka maeneo ya mijini na linalofaa wakaazi muhimu kwao mashambani.

 

Maswali

(a) Ipe taarifa uliyoisoma anwani inayoifaa

(b) “Hali hii imekuwa ya kuhuzunisha.” Ni hali gani inayozungumziwa katika aya ya 1?

(c) Ujuzi wa kutumia Kompyuta unaweza kumfaidi vipi mwanafunzi?  

(d) Mikakati mipya ya kuimarisha elimu kuhusu maswala ya teknolojia inakabiliwa na

vizingiti vipi?

(e) Taja manufaa mawili ambayo mwalimu anaweza kupata kutokana na ujuzi wa teknolojia

ya Kompyuta

(f) Andika msamiati mwafaka zaidi kwa maneno yafuatayo:

(i) Kompyuta

  (ii) Intaneti

 

 

Majibu ya Ufahamu

1.  MAHOJIANO

Mtindo – kichwa

Mada

Muundo wa tamthilia huzingatiwa

Alama za uakifishaji zizizngatiwe ila alama za usemi

Mahojiano yapokezanwe

Lugha rasmi itumike

Mahojiano yasipite mpaka

Mwanafunzi ajieleze kulingana na;

 • Maelezo ya kibinafsi
 • Elimu
 • Tajriba ya kazi
 • Changamoto ya kazi

2.

 1. Mashaka ya kilimo cha mahindi.  
 2. Shilingi elfu saba na mia tatu.
 3. i) Tisho la korogo na vidiri kufukua mbegu.

  ii) Kiangazi.  

  iii) Mvua ya barafu.

  iv) Gharama kubwa.

 4. i) Haikua vizuri kufurahia faida kabla kuuza mahindi.  

  ii) Mungu anao uwezo wa kuleta barafu na kuangalia kustawisha mimea.

 5. i) Kiwango cha chini cha mvua.

  ii) Kushuka kwa bei

 6. Mahindi aliyodhani yameangamizwa na kiangazi au barafu yalinawiri tena.  
 7. i) Malipo ya kustaafu.

  ii) Wataalamu wa kilimo.

 

3.   (a) – malezi

– Wajibu wa wazazi katika malezi

– Jawabu lolote linalogusia juu ya malezi  ( 1×1=al. 1)

(b) (i) – Baba kuona kuwa wajibu wake ni kulea watoto wa kiume tu

  (ii) – Watoto wa kiume kuonyesha kuwa wao ni tofauti na watoto wa kike  (al.2)

(c) Kwa kuhofia kuwa stamfunza tabia za kike  (hoja 1×2=al. 2)

(d) (i) Palikuwa na ugawaji wa kazi ya malezi

  (ii) Watoto walifunzwa sifa kama vile uvumilivu, bidii , utii n.k.

  (iii) Watoto wa kike walifunzwa upishi, ukulima , usafi n.k. (hoja 2×1=al. 2)

(e) Palipotokea jambo ambalo kwa kulipima mama aliona linampita kimo, alimwita baba

kuingilia naye alimwagiza dadake aje atoe suluhisho.  (3×1=al. 3)

 

(f) Sifa- (i) Ushujaa

(ii) uvumilivu  (1×2=al.2)

(g) (i) Chanzo cha chemichemi – kitovu cha maisha/asili

  (ii) Akishachuchuka – ongeza kimo /kua

 (iii) Hulka – tabia/mwenendo/sifa  (3×1= al. 3)

 

4.  (a)  – Sera ya elimu na athari zake  

-Sera ya kusimamia elimu iwepo  

-Mfumo hasi wa elimu

-Masomo ya ziada

*Mada ilenge Elimu maneno yasizidi 6

(b)  -Ina dosari/dosari

-Haiwapi wanafunzi muda wa kutosha wa kula,kucheza,kupumzika na hata

kuchunguza afya na usalama wao

(c)  -Watoto kukosa maadili mema `

-Watoto kukosa furaha na kuchanganyikiwa akili .  

-Watoto kukosa nafasi ya kucheza na kutangamana hivyo kuathiri viungo vya

miili yao kama moyo,mapafu na akili.

-Watoto kuwa wategemezi wasioweza kujipangia na kutekeleza mambo kivyao.

-Wazazi kutotekeleza majukumu yao ya kuwalea na kuwaelekeza watoto kwani mfumo

huu huwaondolea mzigo wa malezi na gharama ya kuwaajiri walezi.

 

(d)  -Wanapaswa kutekeleza majukumu yao ya kuwalea na kuwaelekeza wanao jinsi

wanavyotaka wawe.

-Wawashinikize wanao wahudhurie shule maana kutawafanya wawe wategemezi

wasioweza kujipangia na kutekeleza mambo kivyao.  

 

(e)  (i)Tashhisi-kufukuza ratiba.

(ii )Msemo –Wakiunga mkono  

-Kupiga marufuku  

(iii)Takriri –Kazi nzito nzito 2*2

(f) (i) Huwindwa kitandani

-Kuondolewa kitandani/usingizini bila ana yeondolewa kupenda

-Kulazimishwa kuamka

  ii)  Maadili- Tabia njema /matendo mema

  iii) Kuwashinikiza – Kuwalazimisha /kuwashurutisha

  iv) Wakembe-Wadogo/wachanga  

 

5.   1. Wizi wa wa mali ya umma  

– Vyeo na madaraka kutolewa hivi hivi tu  

– Uuzaji wa stakabadhi za serikali

– Kuiba madawa  

– Kuhonga ili kupata nafasi za kusoma  

– Kuhonga au kutumia undugu ili kupata kazi

– Kutowajibika kikazi

– Kuiba madawa

 

2. – Kufilisisha serikali  

– Kunyima wagonjwa matibabu

– Kuzorotesha maendeleo na huduma muhimu

– Kuelimika watu wasiohitimu na kuacha walio werevu

– Kupandisha vyeo watu wasiostahili  

– Kazi kufanywa vibaya bila uajibikaji  

 

3. – Kuunda tume na kamati za kuchunguza visa vya ufisadi

– Kurudisha mali iliyoibiwa

– Kuwashtaki wahalifu

 

4. – Uhaba wa kazi  

– Uozo wa maadhili katika jamii

– Kuongezeka kwa umaskini

– Tamaa ya anasa na starehe

– Uongozi mbaya wa kitaifa

– Kukosa huruma na uajibikaji

– Kukosa uzalendo  

5. Hongo/ kuzunguka mbuyu/ chai/kadhongo  

6.  Kazi walizopewa

 1. Ufunuo wa siri ya jambo la aibu
 2. Kuenea kwa jambo au habari
 3. Ona wivu
 4. Waliodhuriwa/ walioumizwa

Umeshikilia

 

6.  (a) Ufisadi (al.1 x 1=al.)

  (b) (i) Ajali za barabarani zinasababishwa na kuendesha gari kwa kasi sana

(ii) Kung’olewa kwa vidhibiti mwendo kinyume na masharti ya uchukuzu na

mawasiliano.

(iii) Kuwepo kwa magari mabovu barabarani ambayo hayakutimiza masharti ya ukaguzi.

(iv) Ufisadi wa maafisa wa usalama

(v) Barabara mbovu zenye mashimo

(vi) Matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa madereva wa malori na matrela  *EZ*  

 1. (i) Wananchi wafahamishwe ya kwamba wana jukumu la kuwaeleza walinda usalalam

endapo gari linapelekwa kwa kasi kupita kiasi.

(ii) Wananchi waelimishwe ili wasikubali kuingia kwenye magari ambayo yamejaa

kupita kiasi

(d) (i) Kuwekwa kwa vidhibiti mwendo kwenye magari ya abiria

 (ii) Kuwachukulia hatua wale wanaotoa na kuchukua hongo

  (iii) Kurekebisha baadhi ya barabara mbovu  

  (iv) Kuwekwa kwa mikanda ya usalama kwenye magari

(e) (i) Kung’olewa kwa vidhibiti mwendo

  (ii) Kutokuweko kwa mikanda ya usalama  

  (iii) Gari kwenda kwa kasi zaidi kutokana na kurekebishwa kwa vidhibiti mwendo ( 2 x 1)  

(f) (i) Shida ambayo imedumu muda mrefu bila suluhisho kuliko kiwango kilichokubaliwa  

 (ii) Mashimo yaliyoachwa baada ya madini kutolewa

  (iii) Vifaa vya gari kwenda kwa kasi kuliko kiwango kilichokubaliwa  

  (iv) Urekebishaji

  (v) Kuchukua au kutoa mlungula/rushwa  

  (vi) Tia hamu ya kufanya jambo   (6 x ½ =al. 3 )

 

7.  a) -Ubakaji wa watoto wa kike

 • Kupigwa kwa wanawake na waume zao
 • Kuchomwa kwa wanawake na waume zao
 • Hutukanwa na kubezwa anapojiunga na siasa
 • Huchukuliwa kuwa kinyago cha mzaha na wanavitimbi/ waigizaji

 b) – Hutekeleza wajibu kama mama – kulea familia/ kutayarisha chakula

 • Hufanya kazi ya ofisi ambapo anakabiliwa na migogoro mingi ya kusuluhisha
 • Hurejea nyumbani kutayarisha chajio, kushughulikia kazi za shule za watoto na kuchangamsha familia3x1= 3

 

c) – Kulinda mazingira

 • Ongezeko kubwa la uzalishaji wa chakula
 • Kutoa ajira ya kibinafsi
 • Kuongezeka kwa pato la ndani  

d) Wawe watu wa vitendo sio kupayuka  

e) Kinyago – sanamu

Mabeza – madharau

(f) i) Mbalagha – Utashangaa mja huyu atayabeba vipi?  

 ii) Uhuishi – mara watupwe mabezo ya kila aina  

 

8.   i) Umakinifu wa watu binafsi, vyombo vya habari, sera na utayarifu wa serikali katika

kugharamia shughuli hii  (4×1=ala.4)

ii) Si lugha dhaifu. Hii ni kwa sababu hakuna lugha hata moja ulimwenguni inayoweza kujitisheleza bila kukopa. Hivyo, Kiswahili kinapokopa, hali hiyo haipaswi kuchukuliwa kuwa

ni lugha dhaifu  (ala 3)

iii) – Istilahi zinazokopwa zinafaa zichukuliwe zilivyo katika umbo lao asili na kufanyiwa

marekebisho machache tu

 • pale ambapo istlahi ya asili haiwezi kukopwa, lugha husika ijaribu kubuni msamiati ufaao
 • kiswahili kisikope kiasi cha ku[poteza upekee wake
 • uundaji wa istahili uzingatie mafologia ya kawaida ya lugha (3×1=al 3)

iv) Uundaji wa istilahi katika Kiswahili n.k.  ala 10

v)  a) Dhana – Fikira inayoeleza ambo fulani

b) Takriban – Neno linaloonyesha ukaribiano wa vitu kwa hali au idadi

c) Istilahi – Neno linalowakilisha dhana Fulani katika uwanja maalum wa maarifa k.v.

siasa, uchumi au hisabati

d) mafologia – Tawi la isimu linaloshughulikia uchambuzi wa maneno  (4×1=al.4)

 

9.  (a)   – Haki za wanawake  

– Taasubi ya kiume

(b   -Mwanamke kuumbwa kutokana na ubavu tu wa mwanaume

(c)  – Ya mawazo akilini, kujinyenyekeza na kujidunisha mbele ya mwanamume

– Ni mwiko kudhihirisha tabia za kimabavu

– Hutarajiwa kujilinda heshima kimwili kwa kuhifadhi ubikira wake

– Mahali pake ni jikoni, hasikiki bali aonekanalo

(d)  – Kuhifadhi ubikira mpaka aolewe

– Mwanamke huolewa haoi

– Ndiye mkosaji kila mara

– Nyumbani aonekana tu, asisikike  

(e)   – Wana uhuru wa kutembea na wanawake ovyo

-Wana uhuru wa kujitetea na kupigana

– Mwanamume ndiye huoa

– Yeye hahesabiwi makosa ila mkewe tu kila wakati hulaumiwa kutuze ufahamu

 1. Ondoa nusu moja ( ½ ) kwa kila kosa la sarufi litokeapo mara ya kwanza.

Usiondoe zaidi ya nusu za alama alizotunwa mwanafunzi

Tahajia

Ondoa nusu alama (½) kwa kila kosa la hijai (h) litokeapo mara ya kwanza kwa swali la ufahamu hadi makosa 6 (yaani alama 3)

(f) – Twawashtumu wengine ilhali sisi twabaguana kimaumbile

– Akasemwa vibaya mtaani

– Hupigwa /hushutumiwa

– Wajitolee

10.  Ufahamu

 • Mwanafunzi aliyeambukizwa Ukimwi
 • Ukimwi vyoni
 • Hofu ya kuambukizwa Ukimwi (yeyote moja =al. 1)  

2. Kuwaambukiza wanafunzi wenzake mia moja na ishirini na wanne virusi vya Ukimwi al.2

 

3. Aliambukizwa Ukimwi na mwanfunzi wa chuo hicho ambaye alikuwa akifanya majaribio

ya ualimu shuleni mwao

4.  _ Apewe adhabu ya kifo

   – Atiwe nguvuni maramoja

   – Tayari amekiri kosa lake na hivyo kumfanya awe na hatia  (zozote mbili al. 4)

5.  Maadili hayapo tena katika vyuo vikuu nchini  

6.   – Kupoteza tumaini kabisa/kuwa katika taharuki kuu

    – Daima dawamu/ kwa vyovyote vile

– Kutumia watu wengine kuwatia adhabu kwa kosa lake mwenyewe  (1×3=al.3)

 

11.  1. Nyimbo za jadi zilizokuwa zikiimbwana Manju, Wangoi au waimbaji stadi wa tangu

walipojumuika katika matukio na hafla mbalimbali kama za jando, arusi, matanga, noma n ashangwe zao za maishani (al 2)

2.  – Mawaidha1

– Taathira au jadhba kutokana na sauti tamu ya manju1

– Burudani1  (al 3)

3.  – Uzito wa mawazo maadilifu 1

– Mizani ya sauti ya manju kulingana na lahami, pumzi zake pamoja na madoido katika uimbaji

4.  – Lugha 1

– Umbo 1

5.  Haijaenea na kupamba moto

6.  – Kongamano – mjadala juu ya jambo fulani unaofanywa na mkusanyiko wa watu 1

– Jadhba – Hisia au taathira ya mawazo inayomfanya mtu ajisahau nafsi yake 1

– Farka – tofauti 1

– Awali – Asili, mwanzo 1 (tazama makosa ya hijai/ sarufi – adhibu ½ )

 

12. (a) Madhila ya Chamkosi/masaibu ya Chamkosi/shida za Chamkosi  

 (b) – Husabasiha kifo

– Hufuja mali katika kutibu/umaskini

– Kuacha mayatima

– Kuporomoka kwa ndoa/familia (zozote 2×1=al. 2)

  (c) Uasherati; madharau/mapuuza kwa ushauri (3×1 = al. 3)

  (d) (i)

Baba

Mama

 • Alikuwa baba dume/katili
 • Mreda/sherati/mkware
 • Mshauri mwema
 • Mpole kwa bwanake
 • Mtiifu kwa bwanake
 • Mlezi mwema

(e) Alikata shauri kusomea taaluma ya uelekezi na ushauri ili kusaidia wengine

Maoni; – Uamuzi huu ulikuwa mzuri kwani ungezuia madhara zaidi. ( Dhana alama 2 maoni al. 1)

 (f) (i) Kutumbulia macho – kuangalia bila la kufanya/kukodoa macho.

(ii) Ameumwa na mbuzi – kuugua ugonjwa wa Ukimwi

 

13 .

 1. Uhai unavyoanza
 2. Hatua ya kwanza katika uhai wa binadamu
 3. Kioja cha mwanzo wa uhai n.k.

2. Ana maana ya kujamiana ambapo mamba hutungwa

3. Imani inayokita mizizi ni kwamba mungu huwatumia mume na mke kumwanzishia

binadamu maisha ya duniani

4. Kromosomu humkadiria inadamu  

 1. Rangi ya ngozi yake
 2. Aina ya nywele
 3. Jinsia- kama atakuwa mume au mke
 4. Kiasi cha werevu
 5. Aina ya damu
 6. Utu wake katika maisha ya usoni  

5. Kwa sababu elimu kutoka kwa jamii na mazingara, pekee haifai kitu, lazima ijenge juu ya msingi wa kromosomu

6.- Kunyonya au kutegemea

  -Mamlaka

Hana uhusiano na mama yake

 

14.  (a) Uhusiano wa Ukimwi na kifua kikuu  

(b) Kuchipuka kwa viini vya ukimwi kulikosababisha kudhoofika kwa kinga mwili  

(c) Hupunguza uwezo wa mwili wa mgonjwa kupigana na vijidudu vya maambukizi

magonjwa, kutodhibiti maambukizi ya magonjwa mbalimbali  

– Huwa na nafasi ya kinga mwilini  

(d) Katika baadhi ya nchi maambukizi ya kifua kikuu hufanyika mapema katika umri

mchanga maishani. Hivyo basi kutokea kwa ugonjwa huu mara nyingi husababishwa

kuwepo kwa ukimwi

(e) Ukosefu wa kinga mwilini

(f) Mmoja kati ya watu wawili au watu wenye virusi vya ukimwi hupata kifua kikuu  

– Asilimia 50-60 ya wagonjwa wa kifua kikuu wameambukizwa ukimwi

(g) Maambukizi ya kifua kikuu hufanyika mapema katika umri mchanga

– Maambukizi mara nyingi hayasababishi ugonjwa huu kwa kuwa kinga za mwili

zasitiri maambukizi haya.

– Baadaye viini vyaweza kuwa hai tena na kusababisha ugonjwa

(h) (i) Kukinga  

(ii) Kipindi cha miaka kumi

(iii) Shughuli/jambo la muhimu/haraka  

  (iv) Chembe chembe zinazosababisha ukimwi

 

15.  a)– Elimu na teknologia

  – Umuhimu wa elimu ya teknolojia  

 b) Hali ya kuhuzunisha ni taasisi ya elimu kukosa kutoa wafanyakazi wenye ujuzi tosha,

hasa wa teknologia za kisasa kama kutumia kompyuta kutenda kazi mbalimbali

  c) – Akipata atajiunga na chuo kikuu ambako ataendeleza ujuzi huo wake

– Akikosa nafasi katika chuo kikuu aweza kuendelea na elimu kupitia elimu mtandao

– Mwanafunzi aweza kufanya utafiti wa kina kupitia intaneti  

 

 d) Vizingiti

 • Mitambo na vifaa vya kompyuta ni ghali
 • Kuna ukosefu wa walimu waliohitimu wa somo la kompyuta katika shule nyingi  
 • Tatizo la ukosefu wa nguvu za umeme katika maeneo ya mashambani
 • Wanafunzi na wazazi kutoka vijijini huona somo la kompyuta kama gumu na linalofaa

kwa wanafunzi wa mjini pekee

e) Manufaa ya kompyuta kwa walimu

Kufunza madarasa kadhaa kwa kipindi kimoja bila kuhudhuria darasani

Kufanya utafiti wa hali ya juu kupitia mtandao wa intaneti

f) Kompyuta- tarakilishi  

Intaneti- Mtandao wa mawasiliano wa tarakilishi
Share this:


EcoleBooks | Maswali ya UFAHAMU na Majibu Yake

subscriber

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Accept Our Privacy Terms.*