Share this:

1.   SHAIRI ‘A’.

Umekata mti mtima

Umeangukia nyumba yako

Umeziba mto hasira

Nyumba yako sasa mafurikoni

Na utahama

Watoto Wakukimbia

 

Mbuzi kumkaribia chui

Alijigeuza Panya

Akalia kulikuwa na pala

Kichwani

Mchawi kutaka sana kutisha

Alijigeuza Simba

Akalia na risasi kichwani

ecolebooks.com

 

Jongoo kutaka sana kukimbia

Aliomba miguu elfu

Akaachwa na nyoka

 

Hadija wapi sasa yatakwenda

Bwanako kumpa sumu ?

Hadija umeshika nyoka kwa mkia

Hadija umepitia nyuma ya punda

 

 

SHAIRI ‘B’

Piteni jamani, Piteni haraka

Nendeni, nendeni huko mwendako

Mimi haraka, haraka sina

Mzigo wangu, mzigo mzito mno

Na chini sitaki kuweka

 

Vijana kwa nini hampiti ?

Kwa nini mwanicheka kisogo ?

Mzigo niliobeba haupo.

 

Lakini umenipinda ngongo na

Nendako

Haya piteni ! Piteni haraka ! Heei !

 

Mwafikiri mwaniacha nyuma !

Njia ya maisha ni moja tu.

Huko mwendako ndiko nilikotoka

Na nilipofikia wengi wenu

Hawatafika.

 

Kula nimekula na sasa mwasema

Niko nyuma ya wakati

Lakini kama mungepita mbele

Na uso wangu kutazama

Ningewambia siti miaka

Mingi.

 

(a) Haya ni mashairi ya aina gani ? Toa saabu

(b) Washairi hawa wawili wanalalamika. Yafafanue malalamishi yao

(c) Onyesha jinsi kinaya kinavyojitokeza katika tungo hizi mbili

(d) Ni vipi Hadija :-

(i) Amekata mti mtima ?

 (ii) Amepita nyuma ya Punda (al.2)

(e) Toa mifano 2 ya uhuru wa mashairi kwa kurejelea mashairi haya

(f) Kwa kurejelea shairi ‘B‘ eleza maana ya:-

(i) Mzigo  

(ii) Siri  

(iii) Kula nimekula

 (iv) Niko nyuma ya wakati  

 

 

2.   Sinisumbuwe akili, nakusihi e mwandani.

Afya yangu dhahili, mno nataka amani

Nawe umenikabili, nenende sipitalini

Sisi tokea azali, twende zetu mizumuni

Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?

 

Mababu hawakujali, wajihisipo tabani

Tuna dawa za asili, hupati sipitalini

Kwa nguvu za kirijali, Mkuyati uamini

Kaafuri pia kali, dawa ya ndwele fulani

Nifuateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?

 

Mtu akiwa hali, tumbo lina walakini,

Dawa yake ni subili, au zongo huanoni

Zabadili pia sahali, kwa maradhi yalo ndani

Au kwenda wasaili, wenyewe walo pangani

Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?

 

Mtu kwenda sipitali, ni kutojuwa yakini

Daktari k’ona mwili, tanena kensa tumboni

Visu visitiwe makali, tayari kwa pirisheni

Ukatwe kama fagili, tumbo nyangwe na maini

Nifuateni sipitalini, na dawa ziko nyumbani?

 

Japo maradhi dhalili, kutenguliwa tegoni

Yakifika sipitali, huwa hayana kifani

Wambiwa damu kaliti, ndugu msaidieni

Watu wakitaamali, kumbe ndiyo bunani

Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?

 

Mizimu wakupa kweli, Wakueleze undani.

Maradhiyo ni ajali, yataka vitu thamani

Utete huku wawili, wa manjano na kijani

Matunda pia asali, vitu vyae shamoni

Nifuateni sipati, na dawa zi langoni?

 

Maswali

(a) Lipe shairi hili kichwa mwafaka

(b) Mtunzi alikuwa na lengo gani alipotunga shairi hili

(c) Mbona mshairi hataki kwenda hospitalini  

(d) Eleza umbo la shairi hili (al. 6
(e) Kwa nini mshairi alitumia ritifaa katika ushairi ?

(f) Andika maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa kwenye shairi :-

(i) Dhalili –……………………………………………………………………………………………………………..  

(ii) Azali -……………………………………………………………………………………………………………….  

(iii) Sahali -…………………………………………………………………………………………………………..  

(iv) Tumbo nyanywe  ……………………………………………………………………………………………….

 

3.  WAFULA KABILIANA NA KISU

Ee mpwa wangu,

Kwetu hakuna muoga,

Uoga ukikufikia, huenda ni wa akina mamayo,

Fahali tulichinja ili uwe mwanamme,

Eewe mpwa wangu, kisu kikali ajabu !

Iwapo utatingiza kichwa,

Uhamie kwa wasiotahiri.

 

Wanaume wa mbari yetu,

Si waoga wa kisu,

Wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo,

Wewe ndiye wa kwanza,

Iwapo utashindwa,

Wasichana wote,

Watakucheka,

Ubaki msununu,

Simama jiwe liwe juu,

Ndege zote ziangamie.

 

Simu nimeipokea,

Ngariba alilala jikoni,

 

Visu ametia makali,

Wewe ndiye wangojewa,

Hadharani utasimama,

Macho yote yawe kwako,

Iwapo haustahimili kisu,

Jiuzulu sasa mpwa wangu,

Hakika sasa mpwa wangu,

Hakika tutakusamehe, mwaka kesho unakuja.

 

Asubuhi ndio hii,

Mama mtoto aamushwe,

Upweke ni uvundo,

Iwapo utatikisa kichwa,

Iwapo wewe ni mme,

Kabiliana na kisu kikali,

Hakika ni kikali!

 

Kweli ni kikali!

Wengi wasema ni kikali!

Fika huko uone ukali!

Mbuzi utapata,

Na hata shamba la mahindi,

Simama imara,

Usiende kwa wasiotahiri

Maswali

 (a) Hili ni shairi la aina gani ? Thibitisha  

 (b) Ni nani anayeimba shairi hili na analiimba kwa nani ?

 (c) Toa ithibati kwenye shairi hili kuthibitisha kuwa msimulizi ana taasubi za kiume  

 (d) Taja kwa kutolea mifano mbinu zozote nne za uandishi katika shairi hili

 (e) Taja shughuli zozote mbili za kiuchumi za jamii inayorejelewa katika shairi hili  

 (f) Eleza kwa mifano, uhuru wa kishairi katika shairi hili

  (g) Msamiati ufuatao umetumika kwa maana gani katika shairi hili ?

   (i) Mbari

   (ii) Msununu

    (iii) Ngariba

   (iv) Uvundo

 

 

 

4.   HATIMA YANGU

 

1.  Mke wangu wameshanipoka

Ndugu zangu, wamedai ububu

Wazazi kuzoea kunigombeza

 

2.  Juzi mali lilimbikiza

Furaha lilitanda

Makanwa yalijaziwa

Hoi hoi ikawa desturi

 

3.   Kilabu tulikwenda

Nyama tulichoma

Mahali tulizuru

Tuliteremsha!

 

4.  Leo mambo yamenigeuka

Wao masahibu siwaoni

Matumbo yakaninguruma

Kama radi ya mvua

 

5.  Nyumbani nimebaki pweke

Mke amenitoroka

Watoto wameparara

Skuli kugharamia

Imegeuka balaa belua

 

6.  Ndipo nimeamua

Afadhali kitanzi badala ya balaa

Kumbe kupanga ndiyo maana

Maisha na waasia

 

(a) Eleza mambo muhimu yanayoelezwa katika shairi hili

(b) Fafanua sifa mbili za anayezungumza katika shairi

(c) Dondoa na ufafanue mbinu zozote mbili za lugha katika shairi hili

(d) Eleza maana ya:-

(i) Ndugu zangu wamedai ububu  

(ii) Kumbe kupanga ndiyo maana  

 

 

5. 1. Nitampa nani, sauti yangu ya dhati

  Kwa kipimo gani, ingawa kiwakatiti

  Amefanya nini, la kutetea umati

Kipimo ni kipi?

 

 2. Yupi wa maani, asosita katikati

  Alo na maoni, yasojua gatigati

  Atazame chini, kwa kile ule wakati

Kipimo ni kipi?

 3. Alo mzalendo, atambuaye shuruti

Asiye mafundo, asojua mangiriti

  Anoshika pendo, hata katika mauti

Kipimo ni kipi?

 

 4. Kipimo ni kipi, changu mimi kudhibiti

  Utu uko wapi, ni wapi unapoketi

  Nje kwa mkwapi, au ndani kwa buheti

Kipimo ni kipi?

 

Maswali

 a) Eleza umbo la shairi hili

 b) Taja na ueleze jinsi mwandishi alivyotumia uhuru wa ushairi  

 c) Eleza ujumbe unaowasilishwa na mshairi  

 d) Andika ubeti wa tatu katika lugha ya nathari

 e) Taja bahari tatu zinazojitokeza katika shairi na utoe sababu  

 f) Eleza msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika shairi hili  

i) Katiti  

ii) Gatigati  

iii) Mangiriti  

 

6. KIPI NIKITENDE?

.    Tayari ni sarakani, niambie yote johara,

Mosi nimpe shukrani, kanizaa bira zira,

Wapo haiko hisani, ningefaa kwa uparara,

Kipi takachokitenda, ni nene heko kwa mama?

 

.     Miezi tisa tumboni, yote nina kajinyima,

Kanikopa uchunguni, safari ndefu kazima’

Kama kinda kiotani, kiniasa huyu mama’

Kipi takachokitenda, ninene heko mama ?

 

. Baba siku jana madadi, kawa vingaito mambo,

Kaolewa na asadi, kachalazwa kwa wimbombo,

Kaona – bali jadili, kuchao puani bombo,

Kipi takachokitenda, ninene heko mama?

 

. Kila kuchao zarani, kupalilia kondeni,

Kachanika mpinini, chungu povuka motoni,

Kaviyariya fingani, kinijali jikoni,

Kipi tukachokitenda , ninene heko mama?

 

. Wa siku hizi vijana, wakahujuru nyumbani,

Wengine wao jagina, kawa lofa mutaani,

Hali ukashiba nina, afikapo tu, “kongoni!”

Kipi takachokitenda, ninene heko mama?

. Nawe bwana siwe maya, vita hasha kiwa kombo,

Tena simfanye yaya, ya kikoa ndio mambo,

Simtende ya hizaya, siwe mwao kila jambo,

Kipi takachokitenda, ninene heko mama?

 

. Sasa jamvi nakuja, kisa nimesakarika,

Naomba niliyotaja, tatia manani kaka,

Nenayo yasiwe ngoja, ili nipokee baraka,

Mema nitamtendea, apate futahi pia.

 

Maswali

(a) Eleza umbo la shairi hili  

(b) Kwa nini msanii amshukuru mamaye ?

(c) Ni kina nani wanaokashifiwa na msanii ? Kwa nini ?

(d) Onyesha tofauti katika ujumbe iliyoko katika beti nne za kwanza na mbili zinazofuata

(e) Toa majina mengine yenye maana sawa na haya yaliyotumiwa katika shairi hili :

(i) Mama

(ii) Dawati

(iii) Imara/thabiti

(f) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika kaika shairi:  

(i) Kawa vangaito mambo

(ii) Wimbombo

(iii) Kongoni  

 

 

7.  Soma shairi hili kisha ujibu maswali yanayofuata

MWANAMKE

1.  Namwona yu shambani,

Na jembe mkononi,

Analima,

Mwanamama,

Mavuno si yake,

Ni ya mume wake.

 

2.  Namwona viwandani,

Pia maofisini,

Yu kazini,

Hamkani,

Anabaguliwa,

Na anaonewa.

 

3.  Namwona yu nyumbnai,

Mpishi wa jikoni,

Yaya yeye,

Dobi yeye,

Hakuna malipo,

Likizo haipo.

 

4.  Namwona kitandani,

Yu uchi maungoni.

Ni mrembo

Kama chombo,

Chenye ushawishi,

Mzima utashi.

 

5.   Namwona mkekani,

Yuwamo uzazini,

Apumua,

Augua,

Kilio cha kite,

Cha mpiga pute.

 

6.  Kwa nini mwanamke,

Ni yeye peke yake,

Heshimaye,

Haki anakosa,

Kwa kweli ni kosa

(Muhammed Seif Khatib)

 

7.  (a) “Shairi hili ni la kukatisha tamaa“. Fafanua dai hili kwa kutoa mifano minne  

(b) Eleza umbo la shairi hili

(c) Andika ubeti wa tatu katika lugha ya nathari

(d) Taja tamathali ya usemi iliyotawala katika shairi zima utoe mifano miwili ya jinsi

ilivyotumika

(e) Onyesha mifano miwili ya ubabadume inayojitokeza katika shairi hili

(f) Eleza maana ya maneno yafuatayo jinsi yalivyotumiwa katika shairi:

  (i) mzima utashi

(ii) maungoni  

 

8. KIACHE KINACHONG’AA

Katu siwe na harara, wala moyo kukupapa,

Usichukue hasira, na moyo kutapa-tapa,

Utaharibu na sura, mwishowe uende kapa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Mbeleye kina madhara, kile kinachokukukwepa,

Mbele yake ni hasara, si chema kitakutupa,

Hutaipata ijara, kuchuma ama kukopa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

 

Hicho jangwa la Sahara, si mnofu ni mfupa,

Hakina njema ishara, humtupa mwenye pupa,

Kibovu kama tambara, hupasuka kama chupa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Kitaleta ufukura, si huko wala si hapa,

Kina mengi mazingira, na mbele kitakuchapa,

Sijitie usogora, ukavimbisha mishipa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Si kazi yenye ujira, mshahara kukulipa,

Ya cheo chenye kinara, na heshima wakikupa,

Mbele haina imara, japo leo wajitapa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Japo kazi ya biashara, kutwa wauza makopa,

Uwe mtu na kipara, Mwananchi ama Yuripa,

Bora uwe na busara, fedha tajaza mapipa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

Usione kinang’ara, huku chapiga marapa,

Ukimbilie kupora, moyo wako kukuzipa,

Kitakugeuza chura, mbele yake utaapa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

 

Usitupe sarara, nyuma kisogo kuipa,

Ukaenda kwa papara, kiumbe mbele kitanepa,

Kwanza tumia fikira, uchague njema chapa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Na sisemi masihara, hakika kweli nawapa

Mlio pwani na bara, wa Mufindi na wa lupa

Maneno haya kitara, muarifu na Wachepa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

Tamati niliyochora, ya shikeni si kuepa

Kisha muwe na basira, na Mola kumuogopa,

Kinachokwepa si nyara, ufunge ndani ya kwapa,

Kiache kinachokwepa, mbeleye kina madhara

 

 (a) Eleza hii ni bahari gani ya shairi

 (b) Eleza dhamira ya mshairi

 (c) Fafanua hasara nne zinazoletwa na tamaa – vile ving’aavyo

 (d) Taja na ueleze mbinu mbili za kifasihi zilizotumika katika shairi  

 (e) Andika ubeti wa tano katika lugha ya nathari  

 (f) Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi  

(i) Kuchuma

(ii) Kisogo kuipa

 

9.   Alipokwenda kwao, mamaye alimwambia,

Nipa fedha au nguo, nataka kwenda tumia!

Nikosapo hivi leo, nipa kisu tajitia ! 

Huzunguka akilia kwa maana ya uketo

 

Ndipo mamaye kawaza, pamwe na kuzingatia,

Fedha zako umesoza, na leo zimekwisha,

Kisu sikukukataza, twaa upate jitia!

Mbele zangu n’ondokea! Wende na ukiwa wako!

 

Ulipogeuka nondo, nguo ukazingilia,

Kakaka kwa vishindo, usisaze hata moya,

Leo wanuka uvundo, wambeja wakukimbia!

Mbele zangu n’ondokea ! Wende na ukiwa wako!

Ukijigeuza nyama, kama Simba ukilia,

Watumwa ukawaegema, ukawla wote pia,

Pasi kuona huruma, kutoa wahurumia,

Mbona hukuzingatia? Wende na ukiwa wako!

 

Si mimi naliokupa, ukata huo, sikia!

Kwamba utakuja hapa, nipate kuondolea,

Naapa thama, naapa, sina la kukutendea!

Mbele zangu n’ondokea! Wende na ukiwa wako!

 

 

Tamati, nalikomile, ni hayo nalokwambia,

Hapahitaji kelele na kujirisha mabaya,

Na kwamba yakutukie, sema yapate n’elea!

Zidi radhi kuniwea ! Wende na ukiwa wako!

 

Maswali

 (a) Lipe shairi hili anwani mwafaka

 (b) Ni maudhui gani yanayojitokeza katika shairi hili

 (c) Taja na ueleze tabia za mnenewa katika shairi hili

 (d) Mshairi ametumia uhuru wa utunzi. Taja sehemu mbili alikotumia uhuru huo

  (e) Eleza umbo la shairi hili

 (f) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika shairi :-

(i) Uketo

(ii) Ukata

 

 

10  . Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

Msituni nikakuta, nyuki wamo mzingani,

Kwa juhudi wanakita, mara nje mara ndani,

Husuda wameikata, hata hawasengenyani,

Nyuki ni wadudu duni, wanashinda kwa umoja

 

Mchwa nao nikaona, wamejenga masikani,

Wafanya bidii sana, uvivu hawatamani,

Wao husaidiana, tena hawadanganyani,

Mchwa wadudu wa chini, wanaishi kwa umoja

 

Nalo jeshi la siafu, hutandawaa njiani,

Laenda bila ya hofu, maana ajiamini,

Silaha zao dhaifu, meno, tena hawaoni

Wa kuwatadia nini ? Kwani wanao umoja.

 

Nao chungu wachukuzi, nyama warima njiani,

Masikini wapagazi, mizigo yao kichwani,

Ingawa si wachokozi, wakali ukiwahini,

Katu hawafarakani, wanadamu kwa umoja.

 

Sisi ni wana Adamu, mbona hatusikizani,

Tusitietie hamu, ukubwa kuutamani,

Wachache wataalamu, tuwasadi kwa imani,

Hii “Huyu awezani,” yatuvunjia umoja

 

Maswali

 (a) Lipe shairi hili anwani mwafaka.

(b) Ni sifa zipi nne zinazopewa wanaozungumza.  

(c) Onyesha jinsi mwandishi alivyotumia uhuru wake katika shairi hili.  

(d) Eleza muundo wa shairi hili.

(e) Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari.  

(f) Taja mafunzo mawili unayopata kutokana na wahusika wanaozungumziwa.

(g) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika shairi hilo.

(i) Chungu

(ii) Tuwasadi

 


11.  Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

 

Twamshukuru Mwenyezi. Kamwe wingi ukarimu

Alo na kiti cha enzi, Mola wetu akramu

Kutupa kitu azizi , lugha kutakalamu

Lugha ni kitu kitamu, ujuwapo kutumia

 

Lugha mkuu mlezi , aleaye binadamu

Hata wanyama ja mbuzi, wema lugha wafahamu

Hafuguwa simulizi, izaayo tabasamu

Lugha huwa ni imamu, ujuwapo kutumia

 

(3) Lugha hodari mkwezi, akweaye tata ngumu

Huzifyeka pingamizi, zizushazo uhasama

Ikazidisha mapenzi, wapendanao kudumu

Lugha huyeyusha sumu, ujuwapo kutumia

 

 1. Lugha ndiye mpagazi, mazito kuyahudumu

  Pia hupanga vizazi, pasi mbari kudhulumu

  Aidha hufanya kazi, ikawa mustakumu

  Lugha kwayo ni timamu, ujuwapo kutumia

 

 1. Lugha ni mpelelezi, maovu kuwakasimu

  Huwatowa palo wazi, kashuhudia kaumu

  Yasifiwa na wajuzi, kuwa ni kitu adhimu

  Lugha mkuu hakimu, ujuwapo kutumia

   

 2. Lugha huizuwa kazi, kutatiza mahakimu

  Huwaacha kanwa wazi, wakili kitakalamu

  Muhalifu na jambazi, wakaishinda hukumu

  Urongo huwa timamu, ujuwapo kutumia

   

   

 3. Lugha iwe ni kiongozi, Kizungu au Kiamu

  Iwekapo waziwazi, silabi na tarakimu

  Huyakimu maongezi,yakasikizwa kwa hamu

  Lugha huwa ni muhimu, ujuwapo kutumia.

   

 4. Lugha ni mapinduzi, wanyonge na wajukumu

  Kadhalika ni jahazi, ya nahodha muhitimu

  Kufa maji haiwezi, si vina si miizamu

  Lugha maji zam-zamu, ujuwapo kutumia

 

 

Maswali.

 1. Eleza maudhui ya shairi hili
 2. Eleza muundo wa shairi hili
 3. Andika ubeti wa nne katika lugha ya nadhari/ nadharia
 4. Taja huku ukitoa mifano, mbinu tatu za lugha alizotumia mshairi kuwasilisha ujumbe  
 5. Eleza maana ya msamiati kama ulivyotumika
  1. Azizi  
  2. Uhasimu  
  3. Adimu.  

 

 

12.  Soma mashairi yafuatayo kisha ujibu maswali :-

SHAIRI A:

Tunda la elimu zote, wasema wanazuoni,

Ni kwamba mtu apate, kumtambua manani.

Ndipo hadhi aipate, akumbukwe duniani.

 

Elimu bila ukweli, haizidi asilani

Giza na nuru muhali, katu havitengamani,

Uwongo uje kwa ukweli, itue nuru moyoni.

 

Elimu ni kama mali, haichoshi kutamani,

Ni bora yashinda mali, taji la wanazuoni,

Elimu njema miali, iangazayo gizani.

 

Mtu hachomwi na mwiba, na viatu mguuni,

Ulimwengu una miiba, tele tele majiani,

Elimu ukiishiba, U salama duniani.

 

Wafu ni wasiosoma, watazikwa ardhini,

Hai ndio waulama, wapaao maangani,

Elimu jambo adhima, aso nayo maskini

 

Elimu ina malipo, utayalipwa mwishoni

Pale uitafutapo, ujira usitamani

Mwanachuoni afapo, mbingu huwa na huzuni.

 

Haki ya kuheshimiwa, ni yao wanachuoni,

Wao wameongolewa, na ni taa duniani.

Kweli wanapojua, watoe bila kuhini.

 

Elimu bila amali, mti usio majani,

Haumtii kivuli, aukaliaye chini,

Inakuwa mushkeli, wa kushuri insani,

 

 

SHAIRI B

Inakera moyo

Hii anga ambayo

Huwasonya njiani

Watokao mashambani

Wa kusalimu kwa bashasha

Wanaoshinda kivulini.

 

Chini ya mwembe

Wa umma.

 

Inakera moyo

Hii sebule ambayo

Huwahini mezani

Wagotao nyundo kutwa

Wa kukabili chakula

Wanastarehe daima

 

Chini ya paa

La umma.

Maswali

(a) Pendekeza kichwa kifaacho kwa kila shairi la A na B

(b) Haya mashairi ni ya aina gani?

(c) Taja sifa zozote tatu za kishairi katika shairi B  

(d) Taja mbinu ya lugha iliyotumiwa :-

  (i) Katika mshororo wa mwisho wa ubeti wa saba katika shairi la A  

  (ii) Katika ubeti wa nne wa shairi la B

(e) Fafanua kwa mukhtasari maudhui ya mashairi yote mawili

(f) Andika ubeti wa mwisho wa shairi la A katika lugha nathari

(g) Taja na uonyeshe jinsi idhini ya ushairi ilivyotumika katika shairi la A  

(h) Fafanua maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika shairi:-  

  (i) Maulama

  (ii) Wameongolewa

  (iii) Wagotao

 1. Huwahini

 

 

13. Soma shairi na kisha uyajibu maswali yafuatayo:-

CHEMA HAKIDUMU

Chema hakidumu, kingapendekeza,

Saa ikitimu, kitakuteleza,

Ukawa na hamu, kukingojeleza,

Huwa ni vigumu, kamwe hutaweza.

 

Chema sikiimbi, kwamba nakitweza,

Japo mara tumbi, kinshaniliza,

Na japo siombi, kipate n’ongeza,

Mtu haniambi, pa kujilimbikiza.

 

Chema mara ngapi, kinaniondoka,

Mwahanga yu wapi? Hakukaa mwaka,

Kwa muda mfupi, aliwatilika,

Ningefanya lipi, ela kumzika?

 

Chema wangu babu, kibwana Bashee,

Alojipa tabu, kwamba anilee,
Na yakwe sababu, ni nitengenee,

Ilahi wahhabu, mara amtwee.

 

Chema wangu poni, kipenzi nyanyangu,

Hadi siku hini, Yu moyoni mwangu,

Yu moyoni ndani, hadi kufa kwangu,

Ningamtamani, hatarudi kwangu.

 

Maswali

 (a) Eleza dhamira ya mwandishi

 (b) Fafanua umbo la shairi hili

 (c) Andika ubeti wa kwanza kwa lugha ya nathari

 (d) Taja na kutoa mfano mmoja wa tamathali yoyote ya lugha inayojitokeza katika shairi  

 (e) Taja mbinu nne za uhuru wa mshairi huku ukitolea kila mbinu mfano  

 (f) Eleza maana ya maneno yafuatayo kulingana na vile yalivyotumika:-

(i) Nitengenee

(ii) Ningamtamani

(iii) Ikitimu  

 

14.. Soma shairi na kisha uyajibu maswali yafuatayo:-

1.  Ni sumu, sumu hatari

Unahatarisha watoto

Kwa ndoto zako zako leweshi

Za kupanda ngazi

Ndoto motomoto ambazo

Zimejenga ukuta

Baina ya watoto

Na maneno laini

Ya ulimi wa wazazi

 

2.  Ni sumu, sumu hasiri

Unahasiri watoto

Kwa pupa yako hangaishi

Ya kuwa tajiri mtajika

Pupa pumbazi ambayo

Imezaa jangwa bahili

Badala ya chemichemi

Ya mazungumzo na maadili

Baina ya watoto na mzazi

 

3.  Ni sumu, sumu legezi

Unalegeza watoto

Kwa mazoea yako tenganishi

Ya daima kunywa ‘moja baridi’

Mazoea mabaya ambayo yanafunga katika klabu

Hadi saa nane usiku

Huku yakijenga kutofahamiana

Baina ya watoto na mzazi

 

4.  Ni sumu, sumu jeruhi

Unajeruhi watoto kwa pesa,

Kwa mapenzi yako hatari

Ya kuwaliwaza watoto kwa pesa

Zinawafikisha kwenye sigara na ulevi

Na kisha kwenye madawa ya giza baridi

Barabara inayofikisha kwenye giza baridi la kaburi la asubuhi

 

Maswali

(a) Pendekeza kichwa kwa shairi hili

(b) Fafanua maudhui ya shairi hili

(c) Ni kwa njia gani kinachozungumziwa kinajenga ukuta?

(d) Dondoa tamathali mbili za usemi zilizotumika katika shairi na uzitolee mfano

(e) Eleza umbo la shairi hili

(f) Uandike ubeti wa nne kwa lugha nathari  

(g) Eleza maana ya vifungu hivi vilivyotumika katika shairi ;

(i) Giza baridi

(ii) Yanakufunga katika klabu

 

 

 

 

 

Majibu ya Ushairi

1.  a) (i) Mashairi huru (2X1)ala. 2

ii) Hayazingatii arudhi za betu,vina, mishororo, mizani na kibwagizo (2×1)ala. 2

 

b) i) SHAIRI A – Anamlalamikia Hadija kwa kumuuwa mumewe kwa kumpa sumu.

  ii) SHAIRI B – Anawalalamikia vijana ambao wanamcheka eti amezeeka na kupitwa

na wakati Wanamramba Kisogo  (2×2)ala 4

c) i) Katika SHAIRI ‘A’ – Hadija alidhani kumuua mewe angepata suluhisho lakini badala

yake amejiletea matatizo zaidi. Watu sasa wamemsuta kwa kitendo chake na watoto

wanamsumbua.

ii) Katika SHAIRI ‘B’ – Mshairi anawakejeli vijana ambao wnamramba mzee kisogo

bila kujua kwamba hawataki kupita. (2×2) ala.4

d)i) Amemuua mumewe – Mti mkuu au kichwa cha nyumba.

ii) Anapata shida za Kujitakia – matatizo yamefurika ngyumbani kama mto (ukupita nyuma ya

punda atakutega au kukupiga teke) (2×2)ala.2

e) Inkisari – Nendako – Niendako

– Mwendako – Mnakoenda

– Bwanako – Bwna yako  (1×2)ala.2

 

f) Mzigo – uzee/umri.

  Jiri – Tajriba /Waarifa / Elimu ya maisha.

 Kula nimekula – Ameishi miaka mingi

 Niko nyuma ya wakati
– Amebaki nyuma ne usasa (4×1)ala.4

 

2.   a) – Matibabu ya kiasili | Dawa za asili| dawa za Kisasa.  

b) kuonyesha kuwa dawa asili zinafaa kwa matibabu kuliko za Kisasa. Watu wazirejele.

c) Ana matibau ya kiasili

Hosptiali kuna operasheni ya visu.

Kuna dawa za asili zisizopatikana hospitali. (4X1) ala 4.

d) Beti Sita.

 • Takhmisa| mishoro mitano.
 • Mtiririko – vina bvya ukwapi na utao vinafanana katika beti zote.
 • Mathnawi – vipande viwili.
 • Mizani ni 8,8
 • Lina kiisho – mshoro wa mwisho unarudiwa beti hadi beti katika beti zote. ( 6×1) ala.6

 

e) kupata idai ya mizani inayotakikana

f)   i) Dhalili – Kudharauliwa,nyonge, maskini,dhaifu.

 ii)Azali – zamani.

  iii)Sahali – Urahisi/ wepesi.

 iv)Tumbo nyangwe

 

3.   (a) – Shairi huru  

– Halijazingatia kanunu za utunzi wa mashairi wa kuzingatia arudhi

 (b) – Anayeimba ni mjomba

  – Anayeimbiwa ni mpwa wake

 (c) – Anaambiwa uoga ukimtikia huenda ni wa akina mamaye

  – Alichinjiwa fahali ili awe mwanaume  

 (d) – Chuku – wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo

  – Takriri – kikali

  – Asitiari – upweke ni uvundo

  – Tashhisi – uoga ukifikia

 (e)   – Wakulima – Atapewa shamba la mahindi

    – Wafugaji – Atapewa mbuzi    

 (f)  – Tabdila – aamushwe – aamshwe

– Inkisari – Mme – mwanamme  

– Kuboronga sarufi – Fahali tulichinja tulichinja fahali

 (g)  – Mbari Ukoo ; kikundi fulani

– Msurruu – Anayenuna

– Ngariba – Mtahirishaji

– Uvundo – Harufu mbaya

4.  (a) (i) Amenyang’anywa mkewe

  (ii) Wazazi wake wanamgombeza

 (iii) Alipokuwa na mali marafiki walikuwa wengi. Alikuwa akiwapeleka marafiki klabu na

walifurahia pamoja wakichoma nyama.

 (iv) Mqwandishi hawaoni tena marafiki wote; wameshatoroka. Ana njaa na matatizo

mengi sana.

(v) Amebaki pweke, mke ametoroka na watoto wameparara. Mwandishi hawezi kulipa karo.

Sasa ameamua kujitia kitanzi  (4×1= al.4)

(b) (i) Mbadhirifu –a alitumia mali vibaya

(ii) Mpweke – Ndugu hawamsemezi anaishi upweke

(iii) Mpenda anasa =- Alikuwa akinywa pombe na kukaa sana klabuni  (al. 2 x 3= 6)

(c) (i) Msemo – Balaa belua

(ii) Jazanda – “Juzi” ni wakati uliopita ilhali ‘leo” ni sasa au wakati huu

(iii) Tashbihi – kama radi ya mvua  (2 x 3= al. 6)

(d) (i) Ndugu zangu wamedai ubub – Ndugu zangu wamekataa kusema nami yaani hawanisemezi

kwa hali yangu mpya.


(ii) Kumbe kupanga ndiyo maana- Amegundua kuwa angepanga maisha yake tangu awali

atumie vizuri raslimali alizokuwa nazo badala ya kuzifuja  (2×1= al.2)

5.  a) – Beti nne

 – Mishororo mine katika kila ubet (tarbia)

 – Mshororo wa nne mfupi (msuko)

 – Mizani 6:8 mshororo wa 1-3 kikai

6 mshororo wa mwisho

 b) Inkisari – Anoshika

– Alo

– Asosita

 Lafudhi – Katiti

– mangiriti

 Kutaja 2 mifano 1

 

 c) – Anataka asikike (mawazo yake yasikika)

– Anatafuta atakayoeleza ujumbe wake

– anashindwa atatumia kipimo kipi

– Mtu huyo lazima awe mzalendo aliye jasiri

– Lazima awe anayetambua utu

 

 d) Lugha ya natahria

 Aliye mzalendo na alambuaye haya mtu asiye mwoga, aliyejawa na upendo hata wakati wa

hatari, Ni kipimo kipi cha kumtambua mtu kama huyu

 

 e) tarbia – Mishororo mine kila ubeti  

  Kikai – Mizani isiyozidi 15

  Msuko – Kibwagizo kifupi

 

 f)  i) katili – Kidogo

Gati gati – Ubaguzi

Mangiriti – mambo ya upipi  

6.   a)

 • Beti saba
 • Tarbia – mishororo mine
 • Vina vya ndani na vya nje hubadilika badilika
 • Pande mbili – ukwapi na utao
 • Mizani 8, 8 jumla 16 katika kila mshororo
 • Kibwagizo kipo – kipi titakachotenda, ninene huko mama  

 

b)

Kwa kumza bila zira (chuki)

Kumpenda na kutomuua

Kujinyima yote mazuri kwa niaba yake

Kumtunza mfano wa ndege na makinda wake

Kumtafutia riziki – kufanya kazi (kulima) ili asitaabike

Kumjali

Kutojali visiki katika ulezi wake kama vile baba yake mkali Zozote 5×1=5

c)

 • Vijana ambao baada ya kulelewa na kunenepa hawajali wazazi wao (mama zao)
 • Akina baba wanaowapiga wake wao kwa makosa madogo madogo
 • Pia akina baba wanaowatesa wake wao. Huwafanya yay nyumabni mwao  Zozote 2×1=2

d) katika beti nne za kwanza mshairi anaangazia mema aliyotendewa na mama yake ilihali

katika beti mbili zinazofuata anawakashifu wanaowatendea akina mama wao mabaya Alama 3

e) Mama – nina (Ubeti wa 2)

Dawati – saraka (Ubeti wa 1)

Imara/ thabiti – jahidi (ubeti wa 3)

f)  i) Mambo yakavurugika

 ii) Wimbombo – Kipande cha miti cha kupekecha moto. Chuma cha kupuliziz moto

 iii) Kongoni – Jina la kumkaribisha mtu

 

7.  a) Linakatisha tamaa kwa sababu

 1. Mwanamke anapolima, hafaidiki na mavuno bali yote huchukuliwa na bwanake
 2. Mwanamke hubaguliwa na kuonewa ofisini
 3. Mahali pake ni jikoni, ujakazi n.k lakini halipwi na tena hapewi likizo (hapumziki)
 4. Hutumiwa kama chombo cha mapenzi kukidhia uchuu wa mwanamke
 5. Hamna anayemheshimiwa kwa chochote eti kwa sababu ni mke  Zozote 4 X 1 = 4

b) UMBO

 1. Beti sita
 2. Mishororo sita kwa kila ubeti
 3. Vina vya wisho vya mishororo ya kwanza miwili (mwanzo na mloto) ni –ni- isipokuwa ubeti wa sita (mwisho)
 4. Kila ubeti hususan wa kwanza hadi wa tano umeanza kwa neno Nomwona isipokuwa ubeti wa sita – kupelekea shairi hili kuwa kikwamba
 5. Kila ubeti una kituo tofauti  Zozote 5X1= 5

c) Lugha Nathari

Mwanamke hushinda katika boma akipika, akilea, na hata kufua nguo. Licha ya hayo halipwi na tena hapewi nafasi ya kupumzika  Tuza 4. Tathmini matumizi ya lugha nathari

d) Tamathali iliyotawala

i) Taswira – hali ya kumwona mke nyumbani na kwingineko katika shughuli mbalimbali

k.m  – akiwa nyumbani akipika

 – akiwa kitandani uchi

 – akiwa mkekani katika utungu wa kujifungua n.k.

Kutuza : Kutaja mbinu 1   Mifano 2X1= 2  Jumla 3

e) Mifano ya taasubi ya kiume

 1. Katika ubeti wa kwanza, mume anayachukua mavuno kutoka kwa mkewe
 2. Wanaume katika ubeti wa pili wna ubaguzi na kuonea wanawake

f) Msamiati-  Mzima utashi

 1. Mwenye udiu/ tama kubwa Maungoni

ii)- maumbo, viungo vya mwili vinaonekana wazi

 

8.  (a) – Pindu, kipande cha kiitikio ndicho kianzio cha ubeti unaofuata

  – Tarbia, mishororo minne minne kila ubeti

  – Mtiririko, Vina, vya pande zote vinakeketa- tangia ubeti wa kwanza hadi mwisho(yoyote al. 2)

 

 (b) – Kile ulichojaribu kukifanya hakiwezekani usilazimishe, labda ni mapenz ya Mola.

  – Si vyote ving’aavyo ni vyema, kabla ya kufanya jambo, fikiria/ tumia busara (2×2=al.4)

 

 (c)  – Kuharibika sura

 – Humtupa mwenye pupa

 – Mbeleni utachapwa

 – Huleta hasara

 -Kitakugeuza kuwa kitu kingine kisicho na utu  (zozote 4×1=al. 4)

 

 (d) – Istiari – jangwa la Sahara

  – Semi – Kuvimbisha mifupa, kukipa kisogo (2×2=al. 2)]

 

 (e) Hata ukilipwa mshahara mnono na cheo kikubwa ikiwa mbele kuna majuto kwa sababu

ya majitapo yako, hutafaidi chochote kwa vile mbele utapata madhara  (4×1=al. 4)

 (f) (i) Kuchuma – kupata

  (ii) Kisogo kuipa – Kuikataa/kuiacha (1×2=al. 2)

 

9.  (a) Uketo/uhitaji/ukata/ufukara/umaskini  (2×1=al. 2)

 (b)  – Umaskini

 – Upweke

 – Uwezo

 – Uozo wa jamii

 – Utovu wa nidhamu

 – Ukatili/udhalimu (zozote 4×1= al.4)

 

 (c)   – Mbadhirifu

 – Mwasherati

 – Mlalamishi

 – Kitatange

 – Asiyesikia makanyo

 – Mkata

 – Mtovu wa heshima (Kutaja -1, kueleza -1 = al. 2)  (2×2=al. 4)

 (d)  – Kufupisha maneno (inkisari) nikosapo, nondokea

 – Ritifaa k.m n’eelea

 – Tashbihi k.m. Kama simba

 – Tanakali za sauti k.m. kkka

 – Sitiari k.m. ulipogeuka nondo (1×4=al. 4)

 

 (e) – Beti sita

Mishororo minne minne

Mizani nane nane

Vipande viwili viwili

Mtiririko wa vina vya mwisho, vya kati vikibadilika badilika

Kipokeo (1×4=al. 4)

 

 (f)   (i) Umaskini

 (ii) Umaskini  (1×2=al. 2)

 

 

10.  (a) Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu

(i) Umoja

(ii) ushirikiano (yoyote moja = al. 2)

  (b)   (i) Nyuki wanafanya kazi kwa umoja- Hawasengenyani

   (ii) Mchwa wana bidii/ hawana uvivu

  Mchwa husaidiana na hawadanganyani

(iii) Chungu hawafarakani

(iv) Siafu hujiamini  (zozte nne 4×1=al.4)

  (c) (i) Kubanaga sarufi/ kubananga lugha mfano :-

 – Uvivu hawatamani – hawatamani uvivu

  – Ukubwa kuutamani – kutamani ukubwa

(ii) Inkisari/ufupisho wa maneno

mf. awezani – anaweza nini

(kutaja alama 1 ; mfano alama 1 = ala. 2)

  (d)  tarbia/nne – mishororo minne katika kila ubeti

Ukaraguni – vina vinavyotofautiana kutoka ubeti mmoja hadi mwingine

 •  Kiishio ambacho hakifanani kutoka ubeti hadi ubeti
 •  Liona beti tano
 •  Ni la mathnawi – vipande viwili, ukwapi na utao
 •  Mizani 16 katika kila mchororo, 8,8,  (al. 4)

 

 (e) Mwandishi wa shairi anauliza kwa nini sisi ni wanadamu lakini hatusikizani.

  Huwa tunatamani ukubwa kwa hamu.

  Hata wale wachache ambao ni wataalamu hatuwaamini. Huwa tunasema kwamba hawawezi  

chochote. Mshairi anamalizia kwa kusema kwamaba dharau itatuvunjia umoja  

 (Tathmini majibu ya mwanafunzi  al. 4)

 (f) – Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu

  – Bidii ni ushirikiano kazini

  – Kujiamini katika yale tuyatendayo maishani  (zozote 2×1= ala. 2)

 (g) (i) Chungu – Wadudu wadogo weusi watambao

  (ii) Tuwasadi – tuwasadiki, tuwaamini, tuwakubali.

 

11.  (a) Umuhimu wa lugha:

 – Lugha nikitu (azizi) cha muhimu

 – Lugha hufungua simulizi na kuleta anwani

 Lugha hukuza mapenzi

 – N timamu katika nyanja mbalimbali za kazi

 Huokoa katika kesi  

 Huvuta usikilizaji ikitumiwa vizuri  (zozote 5×1=al.5)

 

(b)   Mishororoinne kila ubeti – tarbia

imegawika katika vipande viwili – mathinawi

– Mizani ni 16 kila mshoro/ukwapi 8, utao 8

– Vina  zi, mu

zi  mu

zi-mu

mu-a

ukara vya mwisho vinatiririka

– beti ni 8

– Kituo – ukwapi – nitofauti

Kibwagizo – utao – una keketo  (Bahari)

(c)  Lugha hufanya kazi ngumu kama mpagazi. Isitoshe hutumiwa kupana ya siku za usoni/zijazo

   bila kudhulumu.Hufana mambo yakanyooka nakwa hivyo ni nzuri unapofahamu na kwa hivyo

    ni nzuri unapoifahamu  

(d)  Jazanda – Lugha mkuu mlezi – ni mpelekezi

 – Lugha ni imamu – ni hakimu mkuu  

Mashairi – Lugha hodari mkwezi – ni jahazi

– Huyeyusha sumu – maji zamu  

– Ndiye mpagazi – zamu

Tashibihi – hata wanyama ja mbuzi

Misemo – huzifyeka pingamizi, huwaaxcha mkamwe

Tashhisi – Izaayo tabasamu

tabaini – Si vina ci milizamu (zozot 3 = 1×3=al.3)

(e)   Azizi – kitu cha thamani

Uhasimu – Uadui, uhasama, hali ya kufarakana

Adimu – Tukufu/ushujaa/jasiri  (al. 3)

 

12.

SHAIRI LA A

SHAIRI LA B

a) Elimu/ elimu ni muhimu

Kero moyoni (alama 2)

b) Tathlitha/ utatu/ ukara

Shairi huru (alama 2)

c)- Lina beti nne

– Idadi ya mishororo hutofautiana katika kila ubeti

– Hakuna urari wa vina

– Hakuna kibwagizo

– Hakuna migao

Hoja 3 = alama 3

 

d) i) Tashhisi/ uhaishaji

ii) Istiara (chini ya paa la umma) yaani starehe alizonazo mwenye mali zinazotokana na jasho la wahitaji

e) Maudhui- umuhimu wa elimu sulubu hawaheshimiwa

Dhuluma dhidi ya wafanyakazi za sulubu k.m. wanapuuza, hawaheshimiwi (alama 4)

f) Mathari

– Elimu isiyo na vitendo ni sawa na mti ambao

hauna majani

– Haumpumzishi yeyote anayekaa chini ya kivuli chake

– Ni taabu tupu udanganyifu kwa watu

 

 

 

 

(alama 3)

g) i) Maulama- Wasomi

ii) Wameongelewa- Wametukuzwa, wamesifiwa (Alama 2)

i) Wagatao- wagongao

ii) Huwahini- Nyima Kataza (alama 2)

 

13. Dhamira ya mwandishi ni kuwa chema hakidumu.

-Shairi lina beti 5

-Kilau beti una mishoro 4 yenye vipande 2.

-kila mshororo una mizani 6, yaani (6 kwa 6) jumla mizani 12 kila mshororo.

-Shairi limetungwa kutumia bahari ya KIKAI na pia bahari ya UKARAGUNI. (Zozote 4×1 =4)

 

 c)Kitu chema hakidumu hata kama kinapendeza ,saa yake ikifika kwa kuponyoka ukawachwa

na hamu ya kukirejea lakini wapi.Ni vigumu kwani hauwezekani. (Alama 4)

 d)Mfano mmoja wowote wa tamathali uliojitokeza katika shairi ni ule wa Balagha/

Istiari/Uhaishaji (alama 2)

 e)-Vina vina badilika badilika.

 -Idadi ya mizani katika kila mishororo ya ubeti wa shairi hili imepunguzwa kutoka 8 hadi 6.

  -Mshororo wa kwanza katika kila ubeti wa shairi hili ni kama kibwagizo au mkarara.

 -Neno chema limetumiwa kubainisha maana tofauti.

 -Aina ya tarbia lakini limetengeka kikai. (zozote 4×1 = 4)

 

 f) (i)Nitengenee, Niweadilifu / niwe mwema / niwe sawa.

  (ii)Ningamtamani – Ningemthamini

  (iii)Ikitimu – ikifika (1×3 = 3

 

14.  a) Kichwa

Kielelezo kibaya

Tabia mbovu kwa watoto

Wazazi wabaya/ walegevu

b) Maudhui ya shairi

Mshairi anasema kuwa wazazi wanahasiri watoto kwa pupa yao ya kulewa kila wakati na kuwa kielelzo kibaya

Wazazi kukaa vilabuni mpaka usiku wa manane bila kufahamiana na watoto wao ni vibaya

Wazazi kuwapa watoto pesa nyingi ni tabia potovu kwani wanazitumia dawa za kulevya

Wazazi wanatafuta utajiri na kukosa wakati wa kuwashauri/ kuwafunza maadili mema

c) Kinachojenga ukuta

Hapana mazungumzo ya kishauri baina ya watoto na wazazi nah ii hujenga ukuta baina ya watoto na wazazi

Kulewa kila wakati na kukaa kilabuni kwa mpaka usiku wa manane hujenga ukuta kwa kuwa mzazi huwa hapati wakati wa kuzungumza na mtoto 2×1=2

d) Tamatahli za usemi

 1. Takriri – ni sumu, sumu
 2. Tashihisi – ndoto zinajenga ukuta/ yanakufunga katika klabu
 3. Istiara – ni sumu Kutaja – 1, Mfano – 1

e) Umbo la shairi

Lina beti nne

Kila mshororo una mishororo tisa isipokuwa ubeti wa mwisho

Ni shairi huru kwa kuwa halizingatii arudhi

 

f) Lugha nathari- ubeti wa nne

 1. Mshairi anasema kuwa wazazi wanaumiza watoto kwa kuwapa pesa
 2. Ni vibaya kuliwaza watoto kwa kuwapa pesa
 3. Kwani huwaingiza katika maovu ya kuvuta sigara na ulevi na mihadarati
 4. Hali hii inaishia upotofu wa watoto/ huwaingiza katika hali mbaya/ kifo

 

g) Maana ya vifungu

 1. Giza baridi – hali mbaya/ kifo

Yanakufunga katika klabu – kuwa na mazoea mabaya ya kukaa kilabuni kulewa mpaka usiku wa manane  
Share this:


EcoleBooks | Maswali ya Ushairi na Majibu Yake

subscriber

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Accept Our Privacy Terms.*