UTUNGAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI

Kwa kawaida mshairi anapotunga shairi au wimbo hutoa hisia au maoni yake juu ya jambo fulani. Mambo hayo hutolewa kufuatana na jinsi anavyoliona jambo lile na anavyoamini kuhusu jambo hilo. Hii ina maana kwamba maoni hayo hutolewa kulenga imani ya mshairi mwenyewe. Imani ya mshairi ndiyo inayojenga msimamo wake katika maisha, yaani falsafa yake.

Mtunzi yeyote katika ushairi, utunzi wake huwa umezingatia vipengele viwili muhimu: fani na maudhui.

Kwa ujumla, mtunzi yeyote wa tanzu ya fasihi simulizi huzingatia vipengele hivi viwili katika utunzi wake.

KANUNI ZA UTUNZI WA USHAIRI WA FASIHI SIMULIZI

Maudhui

Katika kipengele cha maudhui, mtungaji wa mashairi anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo kufanikisha lengo la utunzi wake.

Lengo la mshairi
  • Kabla hajaanza kutunga shairi, lazima ujue sababu za kueleza yale unayotaka; lazima uwe na jambo lililokusukuma kutunga wimbo au shairi.
  • Mshairi anapotunga huwa na kitu maalum akisemacho.
  • Huwa na ujumbe anakusudia kuwasilisha kwa jamii yake.
  • Kuelewa vizuri jamii aliyoiandikia.
  • Mtunzi wa ushairi asitunge bila kuwa na mtu au watu fulani anawakusudia. Watu hao wanaweza kuwa marafiki, watawala, jamaa, maadui au yeye mwenyewe n.k.
  • Utakapo mfahamu unaye muandikia itakusaidia kujua utunzi wake kwa sababu utajua imani na taratibu mbalimbali za maisha ya huyo mtu, na hii itakufanya utunge vizuri kazi yako bila kumdhoofisha mlengwa wako.
Kujua mipaka ya uhuru wa uandishi wako

Mwandishi yeyote huweka mipaka katika uandishi wake. Kwa hiyo mtunzi yeyote atakayependa au asipende, hujikuta amewekewa mipaka katika utunzi wake. Hivyo kama mtunzi, ni muhimu utambue mipaka yako kwani pasipo kufanya hivyo utasababisha matatizo. Iwapo utavuka mipaka, vizuri kutasaidia kuyaandika yale unayoyataka kwa ustadi na kufikisha ujumbe utakayokusudiwa bila matatizo.

Kuoanisha dhamira na wakati

Ni muhimu mtunzi kuandika jambo ambalo anafikiri jamii yake inahitaji kwa wakati huo. Mfano, mtunzi anaweza kuandika juu ya uongozi mbaya, UKIMWI, madawa ya kulevya kwani mambo hayo ndiyo yanayotugusa katika jamii zetu.

Kwa hiyo, kama mtunzi ataandika mambo yanayoendana na mahitaji ya jamii kwa kipindi hicho, atapata hadhira kubwa kuliko akiandika mambo yaliyopitwa na wakati. Mtunzi lazima awe na jambo kuu moja ambalo analitafutia ujumbe mbalimbali na mawazo madogo madogo yatakayokamilisha ujumbe huo.

Fani

Mambo muhimu ya kuzingatia

Kuoana – Utungo wa ushairi ni masimulizi ya tukio fulani au maelekezo juu ya jambo fulani. Hivyo basi, masimulizi au maelezo hayo yanahitaji mtiririko wenye mawazo mazuri yenye kuoana.

  • Utungaji usio na mpangilio mzuri huwa na matatizo kama kukosa kuelewa kile asemacho.
  • Upangaji mbaya wa mawazo husababisha shairi kukosa ladha na hivyo msikilizaji hukosa hamu ya kusikiliza.

Kutotumia mitindo inayofaa

Uchanganuzi wa aina ya shairi atakaotumia mtungaji unategemea sana dhamira iliyo kusudiwa pamoja na lengo alilonalo msanii mwenyewe.

Mfano:

Unapotaka kuzungumza mambo ya kihistoria kwa urefu na upana, inabidi atumie mtindo wa utenzi kuliko wimbo au ushairi kwani utenzi unaweza kutungwa beti nyingi kulingana na kitu kinachozungumziwa.

Utenzi wa lugha

Lugha ni kipengele muhimu sana katika ushairi. Mtunzi wa ushairi katika kipengele cha lugha ni lazima awe makini kwani lugha isipotamu husababisha hata maudhui kuwa chapwa. Mtunzi lazima azingatie mambo yafuatayo katika kipengele cha lugha.

  1. Lugha ya kishairi

Ushairi una lugha yake tofauti na lugha itumiwayo katika mazingira mengine ya kawaida kwani lugha ya ushairi ni ya kutumia maneno machache ya mkato na siyo mengine.

ecolebooks.com
  1. Matumizi ya picha

Hii husaidia kuvuta taswira ya mambo yanapo ongelewa na kukamata akili ya msikilizaji kwa namna ya ajabu. Pia husaidia sana kuvuta hisia na kuleta mguso wa hali ya ajabu na hisia za juu kwa msikilizaji.

  1. Matumizi ya tamathali za semi

Hizi hupanua au hubadilisha maana ya halisi au ya kawaida za maneno ili kuleta maana maalumu iliyo kusudiwa na mtunzi. Mtunzi wa shairi atakapozijenga tamathali zake vizuri huipa uhai na uhalisia zaidi dhana inayoelezwa, huiburudisha na kuzindua akili ya msikilizaji wa shairi na huacha athari ya kudumu katika hisia na mawazo yake.

Tamathali zinazotumika zaidi katika ushairi ni tashbiha, tashhisi, mbalagha, kejeli, sitiari n.k. Hivyo mtunzi wa shairi lazima atumie tamathali kujenga kazi yake.

  1. Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa

Kuna mbinu nyingine za kisanaa zinazo karibiana na tamathali za semi ambazo hutumika sana katika utunzi wa mashairi. Mbinu zinazotumiwa sana ni takriri, tanakali sauti (onomatopea), rithimu (mapigo asilia ya lugha) n.k. Kwa hiyo wakati wa kutunga msanii lazima azingatie mbinu kama hizi.

  1. Matumizi ya nahau na misemo

Hivi ni viungo muhimu katika lugha ya ushairi na hufanya lugha ya msanii au mwandishi fulani kuwa na mvuto mkubwa wa kisanaa. Hivyo ni muhimu kuzingatia matumizi ya nahau na misemo.

  1. Matumizi ya methali

Methali hutumiwa sana na wasanii katika kupitisha hekima na busara kwa jamii na pia hutumika kujenga na kupamba lugha.

  1. Lugha ya wahusika

Tunapozungumzia kuwa kuna lugha ya wahusika, ina maana kuwa kama msanii amekusudia kutoa maonyo basi inambidi atumie lugha ya maonyo. Vilevile kama atatumia hadhira maalum, basi lugha lazima ieleweke na hadhira hiyo.

  1. Kuzingatia kanuni za uandishi

Kuna kanuni zinazotakiwa kufuatwa hasa unapotaka kutunga mashairi ya kimapokeo ambazo ndizo nguzo hasa za ushairi, na pia kuna mambo mengine yanayotakiwa kufuatwa katika kutunga mashairi.

Kanuni za utunzi wa mashairi ya kimapokeo

1) Vina

Katika ushairi, vina ni mizani ya kati na ya mwisho yenye kufanana katika kila mstari wa ubeti. Katika tabia, aghalabu vina hufuatana katika kila mishororo mitatu ya mwisho, lakini inaweza kubadilika.

2) Kituo

Huu ni mstari wa mwisho katika kila ubeti wa ushairi. Kituo cha mstari kinaweza kuwa kimalizio au kiini. Kituo kimalizio kinatumika kulifunga na kukamilisha wazo moja katika kila ubeti. Kituo kiini kina jitosheleza katika kila mwisho wa ubeti na kutaja kwa muhtasari jambo muhimu linalozungumziwa.

3) Kipande

Hiki ni kisehemu kimojawapo katika visehemu viwili au zaidi katika kila mstari, kutegemea na mtunzi mwenyewe alivyoamua kutunga kazi yake.

4) Mizani

Ni jumla au idadi ya silabi zilizomo katika kila mstari wa ubeti. Mizani husaidia kuleta mapigo katika shairi na kufanya liweze kuimbika.

Mara nyingi shairi la kimapokeo huwa na mizani 16 na lazima ifanane katika kila ubeti wa shairi, lakini ushairi wa fasihi simulizi si lazima mizani ifanane sana.

5) Ubeti

Hiki ni kifungu chenye kuleta maana kamili katika jumla ya vifungu ulivyo navyo kwenye shairi. Ubeti hubeba wazo kamili katika shairi.

6) Urari

Mtunzi lazima azingatie kuwa na urari wa mawazo kati ya mstari na mstari au ubeti na ubeti, kwani baadhi ya watunzi hukosea au kazi zao hazina urari wa mawazo au mawazo hayaoni.

7) Utoshelezi

Mtunzi yeyote wa shairi la Kiswahili ni lazima azingatie utoshelezi wa ubeti. Ni lazima kila ubeti ujitosheleze kimaana (ujumbe kabla hujaingia kwenye ubeti wa pili msomaji anapaswa awe ameelewa kile kilichoongelewa kwenye ubeti wa kwanza, na pia mshororo nao inabidi uwe wenye ujumbe).

8) Kuwa na maana

Shairi ni lazima liwe na maana kwani hili ni jambo la msingi katika ushairi. Mtunzi anaweza kufuata kanuni zingine zote lakini bado shairi lake linaweza lisieleweke kwani alikuwa anataka hadhira yake ijifunze nini.

Mtunzi anaweza akagundua beti kumi lakini shairi linakuwa halina maana, na msanii mwingine akafunga hata beti moja tu na shairi lake linakuwa na maana kamili na ujumbe unaoeleweka.

9) Muwala

Ni ufuatanisho wa habari toka ubeti hadi ubeti. Mfano, shairi lenye beti nane linaweza kuleta zama ambapo ubeti wa nne ungekuwa wa pili na wa pili labda ungekuwa mahali fulani au usinge kuwepo kabisa kutokana na mtiririko ulivyo kuwa. Haya yote ni katika kufanya miwala iwe mizuri katika shairi, na hiyo ni moja ya kazi ngumu katika kutunga shairi la Kiswahili.

10) Msisitizo

Hii ni hali ya kushadadia kiini cha jambo au dhamira kuu katika utungo huo. Msisitizo katika shairi linaweza kuwa wima au ulalo.

Baada ya kuona hizo kanuni za mtunzi na shairi, tuangalie mambo mengine muhimu katika utunzi wa shairi ili liwe bora au zuri zaidi, kama:

I. Kutorudia maneno

Shairi litapungua utamu kwa kurudia maneno. Msanii anaporudia neno moja katika kila ubeti husababisha shairi kukosa ladha na utamu, pia mtunzi huonekana kama hana ujuzi wa lugha.

Lakini kuna mashairi ya msisitizo ambayo toka ubeti wa kwanza mpaka wa mwisho huanza na neno hilo basi kama neno huanza na shida basi katika kila ubeti huanza na neno hilo hilo. Hii siyo kurudia maneno bali ni mtindo wa msanii.

II. Kichwa cha shairi

Kichwa cha shairi ni muhimu sana katika kufikisha ujumbe kwa msikilizaji. Kama shairi halina kichwa, linakuwa sio tamu. Shairi bora ni lile linalo kuwa na kichwa.

  1. Kutochanganya dhamira

Pia unapo changanya dhamira mbili au zaidi katika shairi moja, hilo linakuwa shairi baya. Unapoandika shairi, inabidi uende na dhamira moja kuanzia ubeti wa kwanza mpaka wa mwisho, ndipo shairi linapendeza na kueleweka.

  1. Kunga

Siri ya shairi ni kulihifadhi lisiwe mbali sana. Mtunzi anapotunga inabidi asitumie lugha ya kashfa au ya matusi. Anaweza kutumia lugha ya mafumbo ili aweze kuyafumbua.

Matumizi ya tamathali za semi

Hizi hupanua au kubadilisha maana za dhahiri au za kawaida za maneno ili kuleta maana maalum iliyo kusudiwa na mtunzi. Mtunzi wa shairi atakapo zijenga tamathali zake huipa uhai na uhalisia zaidi dhana inayoelezwa, pia huburudisha na kuzindua akili ya msikilizaji wa shairi na kuacha athari ya kudumu katika hisia na mawazo yake.

Tamathali zinazotumika katika ushairi ni tashbiha, tashhisi, kejeli, sitiari, n.k. Hivyo mtunzi wa shairi lazima atumie tamathali katika kujenga kazi yake.

Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa

Kuna mbinu nyingine za kisanaa zinazo karibiana na tamathali za semi ambazo hutumika sana katika utunzi wa shairi. Mbinu zinazotumiwa sana ni takriri, tanakali sauti (onomatopea), rithimu, mapigo asilia ya lugha n.k. Kwa hiyo wakati wa kutunga msanii lazima azingatie mbinu kama hizi.

Matumizi ya nahau na misemo

Hivi ni viungo muhimu katika lugha ya ushairi na huifanya lugha ya msanii au mwandishi fulani kuwa na mvuto mkubwa wa kisanaa. Hivyo ni muhimu kuzingatia matumizi ya nahau na misemo.

Matumizi ya methali

Methali hutumiwa sana na wasanii katika kupitisha hekima na busara kwa jamii na pia hutumika kujenga kejeli kwa kupamba lugha.

UTUNGAJI WA MAIGIZO

Mtungaji yeyote anapotaka kutunga maigizo kuna vipengele mbalimbali ambavyo jamii inapitia vizuri kazi yake na akaweza kubuni mbinu zitakazofanya kazi yake ipendeze na kuvutia, hivyo itakidhi mahitaji ya jamii husika kwa kipindi hicho.

Vipengele muhimu vya kuzingatia katika utunzi wa maigizo

(a) Lengo la mtunzi

Mtunzi lazima aandike maudhui yenye umuhimu katika jamii na yanayoendana na wakati. Msanii mzuri inabidi apange maudhui yake hata kama yakiwa yanahusu Tanzania ya zamani, lazima yawe na umuhimu katika Tanzania ya leo. Pia anaweza kuzungumzia masuala tofauti tofauti ambayo yanaleta maendeleo kwa jamii.

(b) Hadhira inayoandikiwa

Mtunzi lazima ajiulize anaandika kwa hadhira gani kwani hadhira atakayo iandikia ndiyo itakayoamua usanii ni nini na vipi jambo hili ni muhimu kwa mtunzi. Kufaulu au kutofaulu kwa igizo hutegemeana na hadhira yako itakavyo pokea igizo litakalooneshwa jukwaani. Msanii pia inabidi afahamu mawazo ya hadhira yake. Juu ya jambo analotaka kuwasilisha, kama ni tofauti na mtazamo wake, basi atumie mbinu itakayo shawishi wakubaliane nayo.

(c) Utenzi wa vitendo

Msanii anapotunga igizo lazima achague matendo ambayo yatasaidia kulijenga wazo lake. Wazo moja linalotokeza huwakilishwa na matendo mengi ambayo yatasaidia kufikisha ujumbe vizuri vile ulivyokusudiwa hadhira yake ipate kujifunza. Dhamira yake kuu ndiyo itakayo muwezesha achague matendo ya aina fulani.

(d) Ujengaji wa wahusika

Wahusika wa maigizo inabidi wajengwe kutokana na msukumo na migongano iliyomo katika igizo. Maneno, mawazo na matendo yao yapate chanzo kutokana na migogoro hiyo. Kwa namna hiyo wahusika watapata uhalisia na kuvaa uhusika wa kuaminika katika jamii waliyotoka.

(e) Uteuzi wa maneno

Mtunzi wa igizo anapaswa kuchagua maneno kwa uangalifu kwa sababu wakati mwingine mtunzi huwapa wahusika wake maneno mengi kiasi kuwa igizo linakuwa na maneno matupu kuliko vitendo. Matendo yakiwa yamejengwa vizuri huleta maana husika kwa hadhira na maneno machache hupelekea igizo kuwa zuri na la kuvutia.

(f) Uteuzi wa misukumo

Msanii anapaswa achague misukumo itakayoweza kusababisha mitazamo isitokee. Ili jambo litokee, inabidi ajenge pande zote ziwe na misukumo yenye nguvu ambayo italeta matokeo. Kama upande mmoja ni dhaifu, basi hakuna jambo litakaloweza kutokea.

(g) Matendo jukwaani

Mtunzi anatakiwa achukue matendo ambayo yanaweza kuoneshwa katika jukwaa. Igizo lolote haliwezi kukamilika bila kuoneshwa jukwaani ili liweze kuonekana kwa hadhira.

Mtunzi inabidi achague matendo ambayo yanaweza kuonesheka huku yakiambatana na mbinu zingine.

UIGIZAJI WA MAIGIZO JUKWAANI

Maigizo yanapooneshwa kwenye jukwaa huonyesha matendo ya binadamu na maisha wanayoishi kila siku, iitwayo leo.

Katika uigizaji wa maigizo, mambo muhimu ya kuzingatia ni:

a) Jukwaa

Katika maigizo lazima kuwe na jukwaa la kuigizia ambalo ni kitu muhimu katika tanzu hii. Zamani maigizo yalikuwa yanaigizwa nje, lakini siku hizi hutumia majukwaa ya ndani.

Hii ni kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, hata hilo jukwaa la ndani bado ni dhiki kuigiza katika jukwaa hilo.

b) Mazungumzo

Vilevile mazungumzo ya wahusika ni muhimu sana tofauti na maelezo ya mtunzi kwani husababisha igizo kuwa zuri na kuvutia machoni mwa watazamaji.

c) Mavazi

Mavazi ya wahusika ni muhimu sana katika maigizo. Wahusika wanapoigiza wanatakiwa kuonesha watu walivyo, wanavyoishi katika kipindi fulani cha historia au watakavyoishi siku zitakazokuja.

Mavazi wanayovaa yaendane na uhalisia wa maisha ya jamii hiyo na kile kilichoigizwa.

Pia maleba huonesha bayana tofauti za kitabaka zilizopo katika jamii. Kazi ya upambaji hufanywa na mpambaji wa jukwaa au mkurugenzi wa maigizo.

d) Vifaa vya kuigizia

Vifaa vinavyotolewa na mtunzi kwa ajili ya kutumika jukwaani mara nyingi huwa na umuhimu. Mtunzi anatakiwa ahakikishe kwamba vifaa anavyotumia mhusika aoneshe halisi ya lile jambo analowasilisha.

Mfano:

Igizo linataka kuonyesha watu wanavyoishi vijijini.

Hivyo basi ni muhimu vifaa vinavyoteuliwa viwe na uhusiano barabara na uhalisia wa jamii iliyo teuliwa.

e) Jinsi ya kuigiza

Wahusika wanatakiwa watende vitendo kwa hisia kuliko maneno. Mhusika anatakiwa afanye hivyo kama kweli yamemtokea yeye (kumgusa yeye mwenyewe) katika maisha yake. Kwa kufanya hivyo atakuwa amefanikiwa kuvaa uhusika na watazamaji wanapata hisia na kuzama katika kulitafakari igizo hilo.

Mfano:

Mtu anatakiwa aigize kama ana huzuni lakini yeye anatabasamu.

f) Mpangilio wa maigizo

Katika maigizo huwa na maonesho mbalimbali ambayo huweza kujisimamia yenyewe lakini wakati mwingine huingiliana na maonesho mengine kwa ajili ya kukamilishana. Mawazo hayo huweza kupangwa katika sehemu mbili mpaka saba na katika sehemu moja katika maudhui kadhaa hupatikana na ndiyo hutupatia vitendo vya wahusika.

Kwa hiyo kitendo kimoja hutupelekea jambo fulani na mambo yanapokuwa mengi sharti kuwa na uwiano katika kujenga migogoro mpaka kufikia kilele na kupata suluhisho la migogoro hiyo.

g) Maigizo katika maigizo

Tanzu hii ya maigizo wakati mwingine inawezekana kukawa na igizo ndani ya igizo. Katika maigizo ya namna hii kuna igizo ndani ya igizo moja ambalo linakuwa ndani ya akili ya wahusika na mtunzi hupandisha jukwaani na kuoneshwa au watazamaji huingiziwa katika upande wa pili ambao huwa na mambo yanayoshughulikiwa.

Mfano:

Mtu aliye kuwa maskini anakuwa tajiri, mwanafunzi anakuwa daktari au profesa na kuonesha matendo ya huyo profesa, na wakati ikiendelea hivyo, moja huwa limegandishwa.

h) Mwisho wa mchezo

Mwisho wa uigizaji, suluhisho linaweza kupatikana au lisipatikane. Kipindi cha nyuma, mchezo ulikuwa hauishi kwa sababu walikosa njia mbadala ya kuondokea jukwaani, lakini siku hizi watunzi mbalimbali wanaweza kutoa masuluhisho na wakati mchezo unaishia waigizaji huondoka jukwaani kwa amani.

KUIGIZA NGONJERA

Ngonjera ni aina ya ushairi zinazowasilishwa kwa kutumia mazungumzo ya majibizano baina ya watu wawili au zaidi.

Jambo kubwa kabisa katika ngonjera ni kwamba husemwa, haziimbwi kifani na kimaudhui hufuata taratibu zote za ushairi.

Vipengele muhimu vya ngonjera

(i) Dhamira maalumu

Ngonjera huwa na dhamira maalum, yaani hujibu swali. Ngonjera hii imeandikwa juu ya nini? Je, ina usemi kwa waangaliaji wake?

(ii) Wahusika

Ngonjera huwa na wahusika; inaweza kuwa na wahusika wawili au zaidi mpaka wahusika wanne. Mfano, inaweza kuwa na wahusika wawili, mmoja mjuaji na mwingine maalum asiyejua kitu chochote, na mwisho wa ngonjera yule maalumu anakuwa amekubaliana na yule mjuaji.

Watunzi wengi siku hizi wameongeza wahusika zaidi ya wawili kwa sababu mchezo hauwezi kuchezwa bila wahusika, maana wao ndio wana himili hisia zao, wanaakili na kutimiza akili zao katika kutatua migogoro inayo wakabili.

Waandishi hugawanya wahusika wao katika sehemu mbili: mhusika mkuu na wahusika wadogo. Mara nyingi mhusika mkuu huwa mwema na wahusika wadogo huwa wabaya, lakini mtindo huo sio mzuri na ni dhaifu.

(iii) Migogoro

Moyo wa mchezo wowote wa kuigiza, iwe ngonjera au maigizo, upo katika migogoro inayojengwa na mjuaji anajibu kumdokeza yule asiyejua ili aweze kujua na mgogoro upate kuisha.

Mgogoro unaweza kuwa kati ya mtu na mtu, mke na mume, au mtu binafsi au migogoro ya kisiasa n.k.

Migogoro inafanya ngonjera ziwe na uhai na ziweze kutafakariana kiakili na kuamsha shauku ya utafiti unaoambatana na fikra.

Kwa hiyo, uti wa mgongo wa ngonjera ni migogoro, na ngonjera nzuri zaidi iambatane na vitendo ili kuleta uhai zaidi na huleta msisimko katika uonyeshwaji.

(i) Lugha

Lugha ya ngonjera ni rahisi, sanifu na ni ya kisasa. Lugha ya ngonjera hushawishiwa na wakati tuliopo, matatizo yanayoambatana na mazingira pamoja na siasa ya nchi.

Ngonjera huongeza msamiati katika lugha ya Kiswahili kwa wanao zisoma, kuzicheza, na pia kutilia mkazo katika lafudhi na kutamka vyema maneno ya Kiswahili.

Fani hii inawasaidia wachezaji pia waangaliaji kukuza msamiati wao, lafudhi, matamshi na ukakamavu katika kutumia lugha sanifu na rahisi kwa umma.

(ii) Mazungumzo (mjadala)

Ngonjera huwa na watu ambao hujibizana. Mhusika mmoja hutoa hoja ili ajibiwe na mwingine, na mwandishi anayepaswa amwachie mhusika wake aonekane kwamba maneno anayoongea ni ya kwake mwenyewe, siyo ya mwandishi. Mhusika inambidi maneno anayotumia yaendane na kile anachokiwakilisha. Mfano: Daktari mvivu. Pia mjadala utusaidie kumjua mhusika tabia yake, hisia zake, mawazo yake, mazingira yake, wakati anaozungumzia na kutuonesha hali ya mchezo kwa ujumla.

(iii) Muundo

Ngonjera ina muundo ambao kama wa shairi, ingawa kuna tofauti ndogondogo zinazotofautisha ngonjera na shairi. Kutokana na muundo tunaona visa vinavyotiririka, vinavyojengwa kufikia kukua mpaka mwisho.

Lazima mawazo ya mwandishi wa ngonjera yafuatane hatua kwa hatua, yawe na mantiki na mtiririko wa fikra zenye kueleweka.

(iv) Vitendo

Mara nyingi taswira au vitendo huanza kabla ya maneno, vivyo hivyo misisimko inayotolewa na silka zilizojificha kama huzuni, furaha, huanza kuonekana kabla mtu hajaanza kuongea. Matendo yanatusaidia kufahamu anachofanya mhusika kwa sababu matendo na muondoko wa kulima ni tofauti na ya mwalimu n.k., kwani hutofautiana jinsi ya kutumia macho, mikono, uso na hata jinsi ya kuweka mkazo na mlegezo.

Vitendo hutasaidia kujua dhahiri dhamira za ngonjera yenyewe.

(v) Jukwaa na vitu vinavyoonekana wakati wa kufanya ngonjera

Tanzu yoyote ya fasihi simulizi huwa na mahali ambapo inatendekea na huitwa mandhari.

Katika ngonjera pia huwa na mandhari ambayo yanaweza kuwa shambani, sokoni, ukumbi wa mkutano, kijijini au ndani ya nyumba, ofisini n.k., au inaweza kuchanganya mandhari mbili au zaidi kutokana na mwandishi alivyoamua kujenga kazi yake.

Kwenye ngonjera, kitu ambacho hutusaidia kujua mandhari ni maneno ya mhusika mwenyewe na maelezo ya mwandishi au kama linachezwa katika jukwaa ambalo jamii inaweza kuona maigizo hayo.

(vi) Mavazi ya wahusika wa ngonjera

Mavazi ya wahusika katika ngonjera ni muhimu sana kwa sababu yatasaidia katika kufikisha ujumbe wa hadhira husika.

Pia yatatusaidia kutupa mwanga zaidi na kujua wahusika wetu na pia kutupa kazi na nafasi ya wahusika wa ngonjera hiyo.

Vilevile hutusaidia kujua vipindi mbalimbali ambavyo jamii imepita, mfano; mavazi ya kipindi cha ukoloni wa Kiarabu, tofauti kati ya kizazi kimoja na kingine.

(vii) Mwanga na msaada wake katika kuonesha ngonjera

Mwanga husaidia kuunganisha pamoja mambo yote yanayoonekana jukwaani. Pia husaidia kuonyesha nguo, mavazi ya wahusika na vitu vyote vionekanavyo jukwaani na hata wahusika kuweza kuwaona waangaliaji wake.

Mwanga unaweza kuwa mwanga wa jua, mwezi, moto, taa za umeme, kibatari n.k.

Hata hivyo, mambo yote haya hutegemea dhamira hiyo, ngonjera waonyeshaji na hata mavazi ya wahusika.

Pia katika ngonjera huweza kuambatana na muziki au ngoma, hutegemea ngonjera hiyo.

Muda mwingine huweza kuambatana na nyimbo fupi ambayo itasaidia kuonesha hali ya mchezo kwa ujumla, dhamira kusisimua n.k.

Muda mwingine nyimbo inaweza kufuata mwisho wa ngonjera.

TOFAUTI YA MASHAIRI NA NGONJERA

S/NMASHAIRINGONJERA
Shairi huweza kutungwa ili liimbwe kama vile redioni au lisomwe. Ngonjera hukaririwa kwa maneno yenye kuonesha hali ya mazingira.
Shairi huimbwa au kusomwa na mtu mmoja. Ngonjera husemwa na watu wawili au zaidi wanaojadili matatizo mbalimbali.
Maneno ya mashairi hutofautiana kutoka shairi hadi shairi, dini, majonzi, matatizo ya siku za kila siku. Maneno yake hulenga kujibu swali moja.

Mara nyingi mwisho wa ngonjera huishia na mshindi na dhamira itakiwayo.

Ni pia wakati mwingine watu huona kama udhaifu kwani inapasua pande zote mbili zijadiliwe kwa kina na kwa usawa, upande wa kufaulu na kutokufaulu.




');}
Bc0138c3d2dab0944d91d638547c2715

subscriber

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Accept Our Privacy Terms.*